UCHAMBUZI: Maadhimisho ya Kitaifa Kiswahili na Utamaduni yachochee fursa za kiuchumi

Tuesday September 10 2019

 

By GADI SOLOMON

Maadhimisho ya Kitaifa ya Kiswahili na Utamaduni yanayoanza Septemba 12 hadi 14 jijini Arusha, yamebeba dhima ya kukienzi Kiswahili na Utamaduni kama nyenzo ya maendeleo.

Maadhimisho hayo kwa mara ya kwanza yatafanyika kwa ushirikiano wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) na Training Centre for Development Cooperation (MS TCDC).

Maadhimisho hayo yametoa nafasi ya wadau mbalimbali wa Kiswahili na viongozi wa taasisi za Kiswahili kuwasilisha mada mbalimbali.

Baadhi ya watakaowasilisha mada ni Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Profesa Kenneth Simala, Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili (Tataki), Dk Ernesta Mosha.

Pia wapo Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Dk Selemani Sewangi pamoja na Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza), Mwanahija Omary.

Miongoni mwa mada ambazo zitawasilishwa ni Kiswahili na uboreshaji wa maisha ya jamii kupitia elimu kwa umma, Kiswahili na utamaduni katika kuimarisha amani, usalama na umoja. Pia, mada zingine ni; Kiswahili katika ujenzi wa uzalendo wa Afrika Mashariki na utamaduni na fursa za maendeleo endelevu ya mwanamke.

Advertisement

Licha ya mada mbalimbali kutolewa, pia kutakuwa na maonyesho kutoka kwa wadau mbalimbali wa Kiswahili wakielezea uzoefu ufundishaji lugha ya Kiswahili na utamaduni kwa wageni, mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi pamoja na wachapishaji wa vitabu vya Kiswahili.

Maadhimisho hayo ya kitaifa yanafanyika ikiwa ni wiki chache tangu lugha ya Kiswahili ikiwa imepewa nguvu zaidi kimatumizi na wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).

Hii inawapa nafasi wadau na wanataaluma ya Kiswahili kusherehekea kwa pamoja juhudi za Rais John Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano kukijali na kukitukuza Kiswahili. Tukumbuke kuwa tayari Kiswahili ni lugha rasmi kwenye Umoja wa Afrika (AU) na imeshawahi kutumika katika mikutano ya wakuu wa umoja huo.

Hivyo, baada ya Kiswahili kupitishwa imekuwa miongoni mwa lugha tatu ambazo ni Kifaransa, Kireno na Kiingereza ambazo zinatumika.

Watanzania wana kila sababu ya kufanya maadhimisho kwa kishindo kutokana na lugha hiyo kupewa nguvu kutumika kwenye ukanda wa nchi za Sadc ukiwa ni ushawishi ambao umetokana na viongozi wetu nchini.

Tunayo Kamisheni ya Kiswahili ambayo makao makuu yake yapo Zanzibar. Kamisheni hii imekuwa na mchango mkubwa wa maendeleo ya Kiswahili kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia tafiti zake za kitaifa kwa kila nchi, pamoja na mpango wa kubadilisha wataalamu wa Kiswahili.

Watanzania watambue kwamba wanaweza kunufaika kupitia fursa ya kuandika vitabu mbalimbali vya Kiswahili kwa ngazi mbalimbali. Wapo watu wengi ambao tunafahamu ni watunzi wa vitabu, lakini waliigusa jamii bila kujali ngazi za elimu zao.

Maadhimisho hayo ya Kiswahili na utamaduni yaweke msingi mzuri wa watu kutazama fursa mbalimbali kiuchumi.

Kupitia maadhimisho hayo ya Kiswahili, wanafunzi wanaosoma kozi za Kiswahili wajadili changamoto zao. Vilevile wapaze sauti juu ya ajira za Kiswahili kwani wanahitajika wataalamu wengi nje ya nchi lakini hawapelekwi.

Tumechoka kila siku kusikia wimbo wa ajira za wataalamu wa Kiswahili ndani na bara la Afrika, lakini fursa hizo hazionekani kuwanufaisha Watanzania. Ni wakati sasa wa kutazama namna nchi yetu ambayo ndio kioo cha lugha hii inavyoweza kutumia kikamilifu fursa ya kupeleka wataalamu wa lugha nje ya nchi.

Vilevile upande wa utamaduni, tutumie maadhimisho hayo kuenzi lugha ya Kiswahili ambayo inatajwa kuwa moja ya tunu za Taifa letu.

Upande wa pili, hatuwezi kusahau mchango wa mwasisi wa taifa hili kwa kufungamanisha Kiswahili na utamaduni wa Mtanzania.

Tunapoadhimisha Kiswahili na Utamaduni, tutambue pia mchango wa Mwalimu Julius Nyerere katika ujenzi wa jamii ambayo imeunganishwa na lugha moja ya Kiswahili.

Ni lugha iliyojengewa misingi kimatumizi kiasi cha kuzizidi nguvu mamia ya lugha za kikabila zilizosheheni kila kona ya nchi yetu. Tuwashukuru wale waliofanikisha hilo.

Kupitia maadhimisho hayo, liandaliwe wazo la kutoa tuzo kwa viongozi kutambua mchango wa viongozi wa taifa. Ni wazi kwamba wamewezesha Kiswahili kuendelea kutumika katika nyanja mbalimbali za kimataifa.

Gadi Solomon ni mratibu wa mradi wa Swahili Hub

Advertisement