Sabaya apingwa kuzuia fedha Mfuko wa Jimbo, Naibu Waziri afafanua

Monday December 30 2019

 

By Mwandishi Wetu,Mwananchi [email protected]

Moshi/Dar. Mzozo unaoonekana kukua baina ya mbunge wa Hai, Freeman Mbowe na mkuu wa wilaya hiyo, Lengai ole Sabaya umehamia katika fedha za mfuko wa jimbo.

Tayari mkuu huyo ameamua kuchukua ofisi ya mbunge huyo iliyokuwa katika majengo ya Boma na kuikabidhi kwa Idara ya Uhamiaji, akisema kuwa hajawahi kumuona ofisini hapo tangu ateuliwe kuongoza wilaya hiyo.

Na sasa ole Sabaya amezuia fedha za jimbo zilizokuwa zigawanywe kwa kila kijiji Sh500,000 akitaka zikatwe Sh7 milioni kwa ajili ya ujenzi wa choo cha shule, lakini wadau wamempinga.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara alisema hajapokea malalamiko yoyote kutoka kwa Mbowe kuhusu kubadilishwa kwa matumizi ya fedha hizo.

Waitara alimtaka Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), kutoona nongwa kumpigia simu kulalamika kwa vile kwa sasa yeye ni bosi wake.

Juzi jioni, Sabaya alitoa maagizo ya kuzuia fedha hizo za jimbo alizodai zilikuwa zigawanywe Sh500,000 kwa kila kijiji, na kumega Sh7 milioni ili ziende kujenga choo cha walimu kata ya Mnadani.

Advertisement

Shule ya Mijongweni haina choo cha walimu kwa zaidi ya miaka 10 na walimu wamekuwa wakijisaidia katika choo cha zahanati iliyopo jirani na shule hiyo, hali ambayo ilionekana kumkera Sabaya.

Sabaya alizuia mgawanyo wa fedha hizo kwa kila kijiji kwa madai hauna tija, na akasema amemwagiza mkurugenzi wa Halmashauri ya Hai, Yohana Sintoo, kutoa Sh7 milioni leo kwa shule hiyo.

Mwenyekiti huyo wa Chadema, ambaye kwa sasa ana kesi ya jinai inayomlazimisha kutumia muda mwingi jijini Dar es Salaam, jana alikataa kuzungumzia suala hilo akisema muda ukifika atalizungumzia kwa mapana yake na masuala mengine ya jimbo.

Lakini Waitara alisema ingawa hajapokea malalamiko kutoka kwa Mbowe, lakini kuna malalamiko kuwa amekuwa hafiki jimboni na fedha hizo zinakaa muda mrefu.

“Kuna maneno tunayasikia hapo Hai kuwa mbunge huyo anakaa na hizo fedha muda mrefu sana. Kwanza haendi jimboni na usipoenda kwa muda mrefu maana yake hiyo pesa haipitishwi,” alisema Waitara.

Alitolea mfano kuwa mwaka wa fedha uliopita wa 2018/2019 kulikuwa na malalamiko mpaka inaingia fedha ya 2019/2020 ile ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 ilikuwa haijatumika na iko kwenye akaunti.

Waitara alisema kama pesa iko kwenye akaunti muda mrefu na mbunge hajaita kikao, huenda mkuu wa wilaya aliwasiliana na mkurugenzi na kupitia sheria na kuona wanaweza kuzitolea maelekezo tofauti.

“Mkuu wa wilaya anaangalia pia kama kutakuwa na jambo ambalo linataka kutekelezwa kinyume na sheria anaweza kuingilia kati. Fedha hizo za mfuko lazima ziende kuchochea maendeleo,” alisisitiza Waitara.

Hata hivyo, alisema kisheria, msimamizi wa mfuko wa jimbo ni mkurugenzi na si mkuu wa wilaya na kuna kamati yenye wajumbe saba mwenyekiti akiwa mbunge, ndio huamua matumizi ya fedha hizo.

“Yeye kama hawezi kutoa malalamiko bado kuna wajumbe wengine wanasema kwamba sisi bwana tulikaa kwenye kamati tukapitisha matumizi lakini sasa yamekuwa ni tofauti na tulivyopitisha,” alisema.

“Ile fedha haiwezi kubadilishwa bila kamati kuridhia. Ili fedha ziende kutolewa benki, lazima ile kamati ikae na kushauriana na mwenyekiti. Mimi sijapokea malalamiko yoyote.

“Hata kama hawezi kulalamika serikalini, angelalamika kwa Spika, ambaye angeongea na mhimili mwingine kwani hizi ni fedha za Bunge,” alisema Waitara.

Naibu Waziri huyo alitoa mfano wa jimbo la Rombo ambalo mbunge wake, Joseph Selasini aliwahi kulalamikia matumizi ya fedha waliyopitisha kubadilishwa na yeye alishughulikia malalamiko hayo.

Chadema, wanaharakati waja juu

Uamuzi wa Ole Sabaya haujapokelewa vizuri na wadau, ambao wamempinga wakisema sheria haimruhusu.

“Sheria namba 16 ya 2009 ya Mfuko wa Jimbo haijamtaja DC (mkuu wa wilaya) popote, badala yake kuna kamati kwa mujibu wa vifungu kuanzia 7 hadi 10 na mwenyekiti ni mbunge,” alisema mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa.

“Mkuu wa wilaya anaendelea kuufahamisha ulimwengu kuwa sasa Tanzania tunaelekea kabisa kuacha utawala wa sheria na kuendesha nchi kwa matamko ya viongozi.”

Ole Ngurumwa alisema mkuu huyo wa wilaya anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria na akamtaka Mbowe apunguze unyonge na amfungulie Ole Sabaya kesi ya matumizi mabaya ya madaraka.

Kwa upande wake, katibu wa Chadema Kilimanjaro, Basil Lema alisema mkuu wa wilaya si mjumbe wa kamati ya mfuko huo na hana mamlaka ya kuamua matumizi yake.

“Anachofanya Ole Sabaya ni kukurupuka na kulewa madaraka. Lakini pia inaonyesha anatengeneza habari za kuipendezesha CCM kuwa yeye ni mwiba mkali kwa mheshimiwa Freeman Mbowe,” alisema.

Lema alisema kwa mujibu wa sheria namba 16 ya mfuko huo, kamati ikishapanga matumizi ya fedha, haiwezekani kuyapangua.

Hata hivyo, baadaye Waitara alilipigia simu gazeti hili akieleza kuwa amewasiliana na Ole Sabaya ambaye amempa maelezo ya kujitosheleza juu ya uamuzi aliochukua kwa kuwa fedha hizo zilikuwa zinarudishwa Tamisemi.

“Nimeongea na Mheshimiwa DC (Mkuu wa wilaya) amenieleza kuwa kwanza fedha hizo ni za mwaka 2018/2019 na zinapaswa kurudi Tamisemi. Mbowe hajawahi kuitisha kikao kupanga matumizi yake.

“Badala yake, Mbowe alimpigia simu mkurugenzi akimwambia asambaze hizo fedha kila kijiji kipewe Sh500,000. Kamati ina watu saba kama mwenyekiti hayupo, si mtu mwingine angeitisha kikao?” Alihoji Waitara.

Advertisement