Breaking News

Dk Mwinyi: Tumeyabaini yanayotuangusha Pemba

Friday October 16 2020

 

By Kalunde Jamal

Dar es Salaam. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk Hussein Mwinyi amesema wamefanya tathmini na kubaini mambo matatu ambayo huwakwamisha kila wanapofanya uchaguzi mkuu Pemba.

Ameyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na watu kushindwa kujitokeza kupiga kura, kutishiwa amani wakati wa kupiga kura na kutokuwa na mawakala makini.

Amesema licha ya kuwa na wanachama wengi waliohamasika na wanaohudhuria mikutano kwa wingi, wengi wao hawaendi kupiga kura.

Dk Mwinyi aliyasema hayo jana alipofanya mkutano wa kampeni kwa wajumbe wa mashina wa Mkoa wa Kusini Pemba.

Hata hivyo, alisema tayari wameshayatafutia dawa na tathimini inaonyesha CCM inakwenda kushinda Pemba kwa kishindo katika uchaguzi wa mwaka huu.

Alisema ushindi upo, ingawa kuna haja ya kuhakikisha kila mwanaCCM, mwenye kitambulishi cha kupiga kura anapiga kura.

Advertisement

Alisema “wanachama achaneni na dhana ya ‘tutashinda tu’ na kuacha kujitokeza kupiga kura, tusipofanya hivyo kwa kuhamasishana sisi kwa sisi ushindi unaweza usiwe mkubwa kama tunavyotaka,” alisema Dk Mwinyi.

Alisema lengo la mkutano huo ni kuhamasishana kuhusu uchaguzi ambao umekaribia na wao ndio wenye watu, hivyo kila balozi ahakikishe anawatoa wananchi wake kwenda kupiga kura.

“Niwaombe, kwa umoja wenu mhakikishe watu wenu wanakwenda kupiga kura asubuhi na mapema, tutashinda dalili zipo wazi, ila ili uwe ushindi wa kishindo, inabidi tuhakikishe sote tunapiga kura,” alisema Dk Mwinyi.

Alisema jambo lingine walilobaini ni watu kuogopa kwenda kupiga kura kutokana na vitisho, lakini safari hii ulinzi upo wa uhakika.

“Niwatoe hofu wananchi wa Pemba, safari hii hakuna shaka kuhusu ulinzi na usalama, watu wafike vituoni wapige kura bila hofu hakuna kitu kibaya kitakachotokea, nimehakikishiwa hili na sina shaka nalo,” alisema.

Alisema jambo lingine la kufanyiwa kazi ni mawakala waliokuwapo vituoni awali walikuwa dhaifu, hivyo safari hii wawekwe walio madhubuti.

“Sina shaka tutalifanyia kazi hili, nawaamini kwa umoja wenu mtalifanikisha.

Awali, akizungumza katika mkutano huo Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Abdallah Juma Saadallah alisema mabalozi na wenyeviti wa mashina ndio viongozi namba moja wa CCM.

Alisema uongozi uliotukuka unaanza kuchomoza mapema. “Hongera mgombea kwa kuja kuonana nao, hawa ndiyo wapambanaji namba moja wa chama na wamefanya kazi kubwa sana wakati wa uandikishaji vitambulisho vya mpiga kura na vya Mzanzibari mkaazi,” alisema.

Advertisement