Shughuli ya kijamii ya Omjubulo yachelewesha mkutano wa Salum Mwalimu

Muktasari:

Mkutano wa mgombea mwenza wa Urais Chadema Salum Mwalimu umesimama kwa muda kutokana na kuwepo na shughuli ya 'Omjubulo.

Bukoba. Mkutano wa kampeni za mgombea mwenza wa Urais wa Chadema, Salum Mwalimu zimesimama kwa dakika kadhaa kutokana na shughuli ya kijamii ya 'Omjubulo' kufanyika jirani na ulipo uwanja unapofanyika.

Mwalimu alifika katika viwanja vya Kashai Shuleni, Saa 10 jioni leo Jumapili Oktoba 18, na muda mfupi alikaribishwa jukwaani ili akahutubie lakini alipopanda kwenye mimbari akatangaza kuwa hatozungumza hadi muziki uliokuwa ukisika uwanjani hapo uzimwe.

“Hapa tuna mkutano wetu wa kampeni lakini nasikia kuna muziki unalia maeneo ya karibu, sitozungumza mpaka wazime, sheria zipo wazi na nimewaambia polisi ngoja wachukue hatua, wasipozima nitasubiri hata kama ni kesho alfajiri DJ weka muziki nasi tuburudike tukisubiri,” akasema Mwalimu.

Hata hivyo, Polisi kadhaa walionekana wakitoka uwanjani hapo kuelekea mahali ilipokuwa ikifanyika sherehe hiyo umbali wa chini ya mita 50.

Polisi walipofika huko waliwataka watu wale kupunguza sauti ili kuruhusu shughuli mkutano wa kampeni uendelee na baada ya ukimya, Mwalimu alianza kuzungumza lakini sauti ikiwa inaongezeka kidogokidogo kutokea eneo la sherehe, ndipo wananchi uwanjani hapo wakaanza kupaza sauti wakisema wamewasha tena, Mwalimu naye akaacha kuzungumza akanyamaza kimya.

Baada dakika kama mbili kupita, wananchi kwa mamia walianza kutoka uwanjani hapo kuelekea ilipokuwa ikifanyika Omujubulo ambayo kwa wengi ni maarufu kama Kitchen Party.

Baada ya watu kukaribia polisi walianza kuwatuliza watu na Polisi mwingine alisikika akisema, “Tumewaambia mkapuuza sasa huu umati unaokuja mtauweza na hapa mmejaa wanawake watupu, tukisema tuwaache mtapona, sasa zimeni muziki wenu au tuondoke na DJ wenu.”

Dakika hiyohiyo muziki na jenereta vyote vilizimwa na wafuasi wa Chadema walishangilia na kupiga kelele nyingi kisha wakarejea Kashai kuendelea na mkutano wao na pale katika Omujubro alisikia mama mmoja akisema, “Lakini na sisi tuna kibari cha utamaduni” Polisi mmoja alimjibu fuata maelekezo hicho kibali chako kimebatilishwa.

Aidha, Mwalimu wakati akiwanadi wagombea udiwani na Mgombea Ubunge wa Chadema jimbo la Bukoba Mjini, Chief Kalumuna alisema kada huyo wa zamani wa CCM ni miongoni mwa usajili bora kuwahi kufanywa na Chadema 

Wakati Mwalimu anapowasili Bukoba mjini alilakiwa na maelfu ya watu na mamia ya bodaboda na kumsindikiza hadi uwanjani ambako nako alikutana na maelfu ya wananchi waliokuwa wakimsubiri.