45 wakamatwa Dodoma wakiuza mafuta kienyeji, RPC atangaza msako

Wednesday September 18 2019

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto akiwaOnyesha waandishi wa habari madumu yenye mafuta ya petrol na dizeli yaliyokamatwa kufuatia msako uliofanywa mkoani humo kuwakamata watu wanaouza mafuta hayo bila ya kibali 

By Rachel Chibwete, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Polisi Mkoa wa Dodoma nchini Tanzania linawashikilia watu 45 kwa kosa la kuuza mafuta ya petroli na dizeli kwenye madumu kandokando ya barabara.

Pia, Polisi mkoani humo limepiga marufuku biashara ya mafuta ya petroli na dizeli inayofanyika kwenye madumu kwenye makazi ya watu ambayo yamekuwa yakisababisha ajali za moto zinazogharimu maisha ya watu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Septemba 18, 2019 jijini Dodoma, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amesema lita 4,445 za mafuta hayo zimekamatwa.

Amesema biashara hiyo ni hatari kwa kuwa inaweza kusababisha moto kwenye makazi ya watu na kuiingizia Serikali hasara ya kununua dawa bila kupenda.

Kamanda huyo amesema watuhumiwa hao wamekamatwa baada ya jeshi la polisi kufanya msako kwenye wilaya zake zote za mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na wakuu wa polisi wa wilaya na kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao.

“Ukiangalia umri wa watu tuliowakamata ni vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 34 ambao ni nguvu kazi ya Taifa lakini hawataki kufanya kazi na badala yake wanauza mafuta ya petroli kwenye chupa za plastiki ambayo ni hatari sana kwenye makazi ya watu,” amesema Muroto

Advertisement

“Sasa ninawaagiza wenyeviti wa serikali za mitaa na kata ambapo biashara hii inafanyika kuhakikisha wanatoa taarifa mapema vinginevyo wao watachukuliwa hatua za kisheria kwa kuruhusu biashara zisizosajiliwa kufanyika kwenye maeneo yao,” amesema

Kamanda huyo amewataka wananchi kutoa taarifa kwa jeshi hilo wakiona kuna madereva wanaoingia kwenye vituo vya mafuta wakiwa na abiria kwenye magari yao ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Amesema kuingia kwenye vituo vya kujazia mafuta huku wakiwa wamebeba abiria kwenye magari yao ni hatari kwa kuwa kunaweza kutokea mlipuko na kusababisha maafa yatakayosababishia Taifa hasara kubwa.

Advertisement