ACT- Wazalendo yawachagua Mazrui, Bashange naibu katibu wakuu

Mweyekiti wa Act-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu wa chama hicho (Bara), Ado Shaibu. Picha na Salim Shao

Muktasari:

Halmashauri kuu ya chama cha ACT- Wazalendo nchini Tanzania yawachagua Nassoro Ahmed Mazrui  na Joran Bashange kuwa manaibu katibu wakuu wa chama hicho, Tanzania bara na Zanzibar.

Dar es Salaam. Mwenyekiti mpya wa chama cha  ACT- Wazalendo nchini Tanzania, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Nassoro Ahmed Mazrui na Joran Bashange wamechaguliwa kuwa manaibu katibu wakuu wa chama hicho Tanzania Bara na Zanzibar.

Maalim Seif amewatangaza leo Jumanne Machi 17, 2020 wakati akizungumza na wanahabari katika ofisi za chama hicho Magomeni jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia mwenendo wa mkutano mkuu uliohitimishwa juzi Jumapili ambao uliokuwa na ajenda mbalimbali ikiwamo uchaguzi wa viongozi wa juu wa chama hicho.

Mwenyekiti huyo ambaye aliwahi kuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar kuanzia mwaka 2010- 15 amesema manaibu hao walichaguliwa jana Jumatatu Machi 16, 2020 na wajumbe wa mkutano wa Halmashauri Kuu wa chama hicho.

Hatua ya manaibu ilikuja baada ya Ado Shaibu kuchaguliwa na wajumbe 75 wa mkutano huo kuwa katibu mkuu wa pili wa chama hicho akichukua nafasi ya Dorothy Semu aliyekuwa anakaimu nafasi hiyo. Semu kwa sasa ni makamu mwenyekiti wa chama hicho-Bara.

Naye Shaibu amesema katika mkutano huo wajumbe walimpitisha Shaaban Mambo kuwa mshauri mkuu wa chama pamoja na kuunda safu za wajumbe wa kamati 10 za sekretarieti za chama hicho.

Shaibu amezitaja kamati hizo kuwa ni idara ya sera, utafiti,  idara ya uenezi na mahusiano wa umma, idara ya oganaizesheni na wanachama,  idara ya fedha na uchumi, idara ya kampeni na uchaguzi.

Idara nyingine ni pamoja na idara ya haki za binadamu  na makundi maalumu, idara ya amani, idara ya bunge na baraza la wawakilishi na serikali za mitaa, idara ya mambo ya nje na kamati ya maadili.