Afungwa baada ya tetemeko kuua watoto 19

Muktasari:

Mmiliki huyo wa shule anadaiwa kusababisha tetemeko hilo kuua watu kutokana na kujenga jengo la ghorofa la makazi juu ya madarasa na hivyo kuzidi uzito.

Mexico City, Mexico. Mahakama ya Mexico juzi ilimuhukumu kifungo cha miaka 31 jela mmiliki wa shule ambayo watoto 19 na watu wazima saba walifariki baada ya tetemeko kutokea mwaka 2017.

"Tumefanikisha haki kwa waliofariki!" Mwanasheria Mkuu wa Mexico City, Ernestina Godoy Ramos aliandika katika akaunti yake ya Twitter.

Monica Garcia Villegas, kiongozi wa shule binafsi ya msingi ya Rebsamen katika mji huo mkuu wa Mexico alipatikana na hatia ya kusababisha mauaji.

Mahakama pia ilimuamuru mwanamke huyo kulipa jumla ya dola 540,000 za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh1.2 bilioni za Kitanzania) kama fidia kwa familia zilizoathirika, mtoa habari kutoka duru za mahakama aliiambia AFP kwa sharti la kutotajwa jina.

"Sisi, wanasheria na waathirika tunaowawakilisha, tumeridhishwa," Fernando Castillo, mwanasheria wa ndugu waliofariki katika tetemeko hilo, aliwaambia waandishi wa habari.

Mmiliki huyo, ambaye alitoweka kwa zaidi ya mwaka mmoja, ameendelea kujitetea kuwa hahusiki na ana mpango wa kukata rufaa, mwanasheria wake alisema.

Garcia Villegas alikamatwa baada ya kugundulika kuwa alijenga jengo kubwa la makazi juu ya madarasa, hivyo uzito wake unadhaniwa kuwa ulichangia jengo kuanguka.

Shule hiyo ilikuwa ikifuatiliwa duniani kote saa chache baada ya tetemeko la ukubwa wa 7.1 kutokea wakati waokoaji walipoenda kuokoa manusura.

Wanaharakati wanasema upunguzaji gharama uliofanywa na kampuni ya ujenzi, pamoja na rushwa au uwezo mdogo, vilichangia katika kuporomoka kwa majengo wakati wa tetemeko hilo lililoua watu 369.