VIDEO: Alichokisema Mbowe kuhusu Mwanakotide

Mwenyekiti wa Chadema, Freemana Mbowe akitoa heshima za mwisho kwa kada wa chama hicho, Fulgency Mapunda maarufu (Mwanakotide) wakati wa misa ya kumuaga iliyofanyika katika kanisa la katoliki parokia ya moyo mtakatifu wa yesu lililopo Manzese jijini Dar es Salaam leo.

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema aliyekuwa kada wa chama hicho Fulgence Mapunda maarufu Mwanakotide alijitoa kwa chama na nchi yake.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema aliyekuwa kada wa chama hicho Fulgence Mapunda maarufu Mwanakotide alijitoa kwa chama na nchi yake.

Mbowe ametoa kauli hiyo leo Jumatano Oktoba 9, 2019 jijini Dar es Salaam katika ibada ya kuaga mwili wa Mwanakotide aliyefariki dunia Oktoba 6, 2019 katika hospitali ya St Monica alikokuwa amelazwa kwa matibabu.

Katika ibada hiyo iliyofanyika Kanisa Katoliki Manzese, Mbowe amesema Chadema wataendelea kutambua mchango wa  mtunzi na mwimbaji huyo wa nyimbo za hamasa za chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, aliyejizolea umaarufu kupitia mikutano ya hadhara, zikiwemo kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na 2015.

"Tunamshukuru sana Mapunda ametufanyia kazi kubwa tunaiheshimu na tutaienzi," amesema Mbowe na kutoa pole kwa familia na wana Chadema wote kwa kuondokewa na mpendwa wao.

Amesema katika muda mfupi wa maisha yake, Mapunda ameacha alama kubwa kutokana na mchango wake kwa kutumia sauti yake kuimba nyimbo za ukombozi na kuhamasisha mabadiliko.

"Katika maisha yetu haijalishi umeishi miaka mingapi bali umeweka alama gani katika miaka uliyoishi," amesema Mbowe.