Bashiru aanza ziara Kigoma, Zitto Kabwe azuiwa kufanya mkutano

Friday January 17 2020

Katibu mkuu wa CCM Dkt. Bashiru Ally akisaini

Katibu mkuu wa CCM Dkt. Bashiru Ally akisaini kitabu katika ukumbi wa Chama hicho baada ya kuwasili mkoani Kigoma kwaajili ya ziara yake ya siku tatu. Picha na Happiness Tesha. 

By Happiness Tesha, Mwananchi [email protected]

Kigoma. Wakati mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe akizuiwa kufanya mkutano wa hadhara na Jeshi la Polisi mkoani Kigoma leo Ijumaa Januari 17, 2020, katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ameanza ziara ya siku tatu mkoani humo.

Polisi mkoani Kigoma kupitia barua ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kigoma, M.R Mayunga yenye kumbukumbu namba KIG/A.24/60/VOL.1/114 ya Januari 16, 2020, wamemzuia  Zitto kufanya mkutano wake leo kwa sababu za usalama na taarifa za kiintelijensia.

Akizungumza na Mwananchi leo katibu wa CCM mkoa wa Kigoma, Kajoro Vyohoroka amesema baada ya kuwasili mjini Kigoma, Dk Bashiru ataelekea eneo la Kazuramimba  Wilaya ya Uvinza kwa ajili ya vikao vya ndani na viongozi wa chama na jumuiya zake.

“Jumamosi Januari 18, 2020 Katibu mkuu atapokea taarifa ya utekelezaji wa ilani na kazi zilizofanyika kwa kipindi cha miaka minne katika jimbo la Kigoma Kaskazini inayoongozwa na Peter Serukamba (CCM),” amesema Vyohoroka.

Kwa mujibu wa katibu huyo, Jumapili  Januari 19, 2020, Dk Bashiru aliyetokea katika ziara mkoani Tanga na kuwapokea madiwani wanane wa CUF waliojiunga CCM, atakuwa na kikao cha ndani na mabalozi wa CCM na viongozi wa chama hicho tawala na jumuiya zake.

Akizungumzia kuzuiwa kwa mkutano wa Zitto, katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano na Umma wa ACT-Wazalendo,  Ado Shaibu amesema sababu zilizotajwa na polisi hazina mashiko na zinalenga kumzuia Zitto asitekeleze majukumu yake halali ya kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo.

Advertisement

Shaibu amesema mkutano huo ulipangwa kufanyika katika viwanja vya Mwanga Center manispaa ya Kigoma Ujiji.

Advertisement