CAG: Serikali ya Tanzania inadaiwa Sh2 trilioni na mifuko ya hifadhi za jamii

Muktasari:

  • Serikali inadaiwa zaidi ya Sh2 trilioni na mifuko ya hifadhi za jamii, sehemu ya kiasi hicho ilitakiwa iwe imelipwa mwaka wa fedha 2017/18. Amesema ucheleweshaji huo umeathiri uendeshaji wa mifuko hiyo.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inadaiwa Sh2.39 trilioni na mifuko sita ya hifadhi za jamii ambapo kiasi cha Sh1.62 trilioni sawa na asilimia 68 kilipaswa kiwe kimelipwa katika mwaka wa fedha wa 2017/18.

Hayo yamebainishwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwenye ripoti yake ya ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka 2017/18 ambayo pia iliwasilishwa jana Jumatano Aprili 10, 2019 bungeni jijini Dodoma.

Katika ripoti yake, CAG amebainisha kwamba mikopo mingine iliiva tangu mwaka 2014. Amefafanua kwamba kuchelewa kulipwa kwa mikopo hiyo kumeathiri uendeshwaji wa mifuko husika.

CAG ametaja mifuko hiyo kuwa ni Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Mifuko ya Pensheni, ikiwamo Mfuko wa Pensheni wa LAPF, Mfuko wa Pensheni wa Sekta ya Umma (PSPF), Mfuko wa Taifa wa Mafao ya Watumishi wa Serikali (GEPF), Mfuko wa Pensheni kwa Mashirika ya Umma (PPF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

“Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umebeba madeni ya mifuko iliyoungana ambayo yanaweza kuhatarisha ukwasi wa mfuko huu.

“Mapendekezo ya kikokotoo kipya cha pensheni yalisababisha ongezeko la wastaafu wa hiyari kutoka wastaafu 2,562 mwaka 2016/17 mpaka wastaafu 4,730 mwaka 2017/18,” amesema CAG kwenye ripoti hiyo.

Pia, CAG amebaini kwamba mifuko iliwekeza kiasi cha Sh55.17 bilioni katika Benki M na Sh3.15 bilioni katika Benki ya Covenant. Hata hivyo, anasema leseni za benki hizo zimefutwa na Benki Kuu ya Tanzania. Amesema Benki ya Azania imechukua mali na madeni ya Benki M wakati Benki ya Covenant ipo katika hatua ya kufilisiwa.

Katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), CAG amebaini kupungua katika ukuaji wa akiba ya mfuko mwaka hadi mwaka kutokana na ongezeko la gharama za malipo kwa huduma ya afya inayotolewa kwa wanachama wa hiyari ikilinganishwa na mapato yanayokusanywa kutoka kwa wanachama hao.

“Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unapaswa kuchukua hatua stahiki kuhakikisha mtaji wa mfuko unaongezeka,” amesema CAG kwenye ripoti hiyo.