Chadema, CCM watuhumiana mkoani Morogoro

Muktasari:

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimedai baadhi ya wanachama wake wamejeruhiwa baada ya kuvamiwa na wanachama wa CCM katika kitongoji cha Mkuyuni wilayani Kilombero mkoani Morogoro.

Morogoro. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimedai baadhi ya wanachama wake wamejeruhiwa baada ya kuvamiwa na wanachama wa CCM katika kitongoji cha Mkuyuni wilayani Kilombero mkoani Morogoro.

Kimesema hali hiyo imetokea baada ya wanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania kuhoji  sababu za mgombea wao wa uwenyekiti kitongoji cha Mkuyuni, Pius Chitikila kutishiwa na mgombea wa  CCM, Kassim Malawa.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Novemba Mosi, 2019 mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Kilombero,  Shabani Mikongolo amesema vurugu hizo ziliibuka  baada ya Malawa kutoa vitisho kwa familia ya mgombea wa Chadema.

Amesema Malawa alidai hakuna mgombea mwingine katika kitongoji hicho zaidi yake.

Mikongolo amesema baada ya vitisho hivyo baadhi ya viongozi wa Chadema walikwenda nyumbani kwa mgombea huyo wa CCM kutaka kujua sababu za kutoa kauli hiyo.

Amedai kabla ya kufika katika nyumba ya mgombea huyo lilitokea kundi la vijana na kuanza kuwashambulia, kuwapora simu na fedha.

Amesema viongozi wa Chadema waliojeruhiwa ni katibu wa jimbo la Mlimba,  Tumaini Mwakalasya;  mjumbe wa kamati tendaji ya jimbo hilo,  Erasto Mwasajone na katibu wa tawi la Chinaso,  Enesius Msoma.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilombero,  Clarence Mgomba amesema Chadema wamepata taharuki baada ya kuona CCM kinakubalika katika maeneo mengi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa alipoulizwa kuhusu suala hilo amesema hana taarifa na kuahidi kulitolea ufafanuzi atakapopata taarifa.