Chadema yaahidi ruzuku pembejeo za kilimo

Muktasari:

Mwalimu aliyasema hayo juzi katika mikutano yake ya kampeni aliyoifanya katika Jimbo la Kalambo, mkoani Katavi.

Rukwa. Mgombea wa kiti cha makamu wa rais wa Tanzania kupitia Chadema, Salum Mwalimu amesema chama hicho kikishinda uchaguzi Oktoba 28, wanakwenda kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuweka miundombinu ya umwagiliaji na kutoa ruzuku kubwa ya pembejeo za kilimo.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kutaka Watanzania waanze kulima kilimo chenye tija kitakachosaidia kukuza uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla.

Mwalimu aliyasema hayo juzi katika mikutano yake ya kampeni aliyoifanya katika Jimbo la Kalambo, mkoani Katavi.

Kutokana na Chadema kutokuwa na mgombea ubunge jimboni humo, Mwalimu alitumia mikutano hiyo kumuombea kura mgombea urais wa chama chake, Tundu Lissu na wagombea udiwani katika kata zote.

Mwalimu alisema katika utawala wa chama hicho hakutakuwa na ulazima wa kuuza mazao kwenye vyama vya ushirika.

Mwalimu alisema badala yake wakulima wataruhusiwa kuuza mazao yao popote ili mradi tu muuzaji alipe kodi.

“Sera ya chama chetu inaamini katika soko huria, wenzetu CCM wanaamini katika ujamaa, wao wanaamini Serikali inatakiwa kumiliki mali ndiyo maana wananunua ndege badala ya kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wa nchi hii,” alisema Mwalimu.

Alisema Serikali yao itatoa ruzuku ya pembejeo na kuboresha miundombinu ya umwagiliaji kwa kutumia vyanzo vya maji vilivyopo na itarejesha gharama za uwekezaji huo kupitia kodi za wananchi.

Alisema wananchi wakivuna kwa wingi wataongeza matumizi, hivyo kulipa kodi zaidi kwa njia tofauti.

“Toa mbolea bure, boresha umwagiliaji, wakulima wavune tani na tani, weka soko zuri la mazao, wakulima wauze kwa wingi wataongeza matumizi yao ya kawaida nawe kama Serikali unanufaika na uwekezaji wako kupitia kodi,” alisema.

Mwalimu alisema wananchi wasitegemee CCM itabadilika katika hilo, kwa kuwa hiyo ndiyo itikadi yake lakini katika utawala wa Chadema, kampuni zitanunua mazao kwa kushindana na kutoa manufaa makubwa kwa wakulima.

“Katika utawala wetu kampuni zitakuwa zinakuja hapa (Kalambo) kushindana kununua mahindi yenu, nanyi mtamuuzia yule mnayeona anawapa bei nzuri, hizo Amcos kama nazo zitataka kununua zitakuja kununua kwa kushindana na kampuni na hakutakuwa na mkopo, watu watalipwa taslimu,” alisema Mwalimu.

Aliongeza kuwa anafahamu wakulima wa jimbo hilo wanadai Sh315 milioni ambazo waliuza mahindi yao na hawajalipwa na endapo watakichagua chama hicho kuongoza nchi, fedha hizo zitalipwa kwa kuwa ni wizi.

Aidha, Mwalimu aliwahimiza wananchi waliohudhuria kampeni zake kujitokeza kwa wingi Oktoba 28 kuipigia kura Chadema ili iwe mwisho wa changamoto mbalimbali wanazozilalamikia.

“Hiki si kipindi cha kulalamika tena, ni kipindi cha kuchukua hatua kwa kubadilisha kiongozi aliyekuwepo. Kama unalalamika halafu unachagua yuleyule unajidanganya mwenyewe,” alisema.