DC Mbeya ataka Nida kufanya kazi Jumamosi, Jumapili

Friday January 17 2020

 

By Yonathan Kossam, Mwananchi [email protected]

Mbeya. Siku tatu kabla ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzima laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole, mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika ameiagiza Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida)  kufanya kazi Jumamosi na Jumapili.

Akizungumza na wananchi leo Ijumaa Januari 17, 2020 katika ofisi za mamlaka hiyo wilayani humo, Ntinika amesema siku zilizobaki ni chache na zinaangukia siku ya mapumziko, ni vyema Nida ikafanya kazi katika siku hizo.

Amesema ofisi za mamlaka hiyo zinatakiwa kufunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 Jioni au zaidi.

"Ikitokea hadi saa 12 watu bado wapo huduma ziendelee, lakini pia kompyuta za kusomea namba ziongezwe," amesema.

Ofisa msajili wa Nida Mkoa wa Mbeya,  Aluvuya Ntalima amesema watahakikisha wanayafanyia kazi maagizo ya mkuu huyo wa Wilaya ili kuhudumia wananchi kwa wingi.

"Tayari tumeshaongeza kompyuta za kusomea namba na kuongeza eneo jingine kwa ajili ya kazi hiyo," amesema.

Advertisement

Wananchi wanaendelea kuongezeka katika ofisi hizo za Nida kwa ajili ya kupata namba na wengine kupiga picha huku matumaini ya watu wote kufanikiwa yakizidi kudidimia zikiwa zimebaki siku tatu pekee.

Advertisement