Dk Kigwangalla atumia Instagram kumwomba Gambo awasamehe waliosambaza picha za Ngorongoro

Sunday February 23 2020

 

By Muyonga Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Dk Hamis Kigwangalla amewaombea msamaha waongoza utalii ambao walisambaza video kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha uharibifu wa barabara kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Kupitia akaunti yake ya Instagram, Dk Kigwangalla ameandika kuwa amemuomba Mkuu wa mkoa wa Arusha Nchini Tanzania, Mrisho Gambo na kamati ya ulinzi kuwasamehe na kuchukulia hilo kama onyo.

Kigwangalla amesema kwa kuwa ni tukio la kwanza, amempongeza Gambo kuingilia kati suala hilo ambalo ameeleza linalinda hadhi ya nchi.

“Hivi tour guide anayetangaza kwamba Ngorongoro hakupitiki anapata faida gani? kama wageni wakiacha kuja Waziri nanyimwa mshahara ama posho zangu? Ama ni yeye atakayekosa biashara? Watanzania tukae kimkakati jamani,” ameandika.

Amesema ni vema taarifa kama hizo wawe wanazifikisha mahala husika ili zipatiwe ufumbuzi na ikishindikana afikishiwe Waziri moja kwa moja.

 

Advertisement

 

“Ni vema taarifa za changamoto zikafikishwa kwetu kwa njia sahihi. Kama mtu hawapati watu wetu wa huko chini, mimi napatikana kila kona, sijajifungia kwenye selo na sijabadili namba zangu! Nipe taarifa zako na nakuhakikishia nitachukua hatua stahiki na kwa wakati,” ameandika Kigwangalla.

“Huwa sipuuzi taarifa wala ushauri na siangalii umetoka kwa nani. Nafanyia kazi kila kitu. Na ndiyo maana hata majangili tunawakamata kila siku. Kweli tuna uhuru wa kusema na kufanya lolote, lakini tuutumie vizuri kwa maslahi mapana ya Taifa letu. Hii ni nchi yetu sote, tuilinde, tuipende, tuijenge, tuifaidi,” ameandika.

Katika hatua nyingine, Kigwangalla amefanya ziara ya kukagua hali ya barabara za eneo la Ngorongoro kufuatia mvua kubwa kunyesha kwa muda mrefu na Ziwa Magadi kufurika na maji yake kukutana na swampo ya Ngoitoktok.

Amefafanua kuwa wataalamu wa Mamlaka wakishirikiana na wa Wizara wamefanikiwa kuikarabati barabara na sasa hakuna gari zinazokwama.

“Tunajenga barabara ya kutokea eneo la msitu wa Lerai kwa kiwango cha changarawe, sema tumeamua kuinyanyua juu zaidi japokuwa ujenzi umekuwa mgumu kwa sasa kutokana na uwepo wa maji mengi na pia mvua zisizokatika. Kimsingi barabara hii imefungwa kwa sasa japokuwa baadhi ya waongoza watalii wanalazimisha kupita huku kwa kuwa ni eneo lenye faru na simba wengi wanaoonekana kiurahisi. Kwa bahati nzuri kwa sasa eneo hili linapitika bila shida,” amesema Kigwangalla.

Advertisement