Fisi wageuka tishio Geita, waua watoto watano

Tuesday March 24 2020

 

By Rehema Matowo, Mwananchi [email protected]

Geita. Watoto watano wamekufa baada ya kuliwa na fisi  wilayani Nyang’wale Mkoa wa  Geita tangu Januari 2020 akiwemo Nile Hassan mwenye umri wa miaka mitano.

Akizungumza leo Jumanne Machi 24, 2020 mkuu wa Wilaya  hiyo, Hamimu Gwiyama amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo na kubainisha kuwa baadhi ya wananchi wamehamia kwenye maeneo ya milimani ambako ndiko kwenye fisi hao.

Amebainisha kuwa changamoto inayowakabili ni ukosefu wa wataalamu wa wanyamapori na kuwataka wananchi kutoshirikisha fisi na ushirikina.

“Sisi tumetoa taarifa mkoani kuomba watusaidie tupate ofisa wanyamapori ambao watawafukuza hawa fisi kutoka kwenye makazi ya watu warudi mlimani zaidi. Mara nyingi wananchi wenyewe wanaamua kuingia na kuwafukuza fisi ili kujiokoa,” amesema Gwiyama.

Diwani wa Shabaka,  Mageni Mageni amesema katika kata hiyo watoto wanne wameliwa na fisi na kwamba wananchi wamechoka na hawatakuwa tayari kuvumilia.

 “Nimepeleka kilio halmashauri kuomba ofisa wanyamapori aje huku ashirikiane na wananchi kuua fisi lakini hadi sasa hakuna aliyekuja na watu wanaendelea kupoteza watoto sasa tumesema basi tutawavamia hao fisi sisi wenyewe,” amesema.

Advertisement

Ofisa tarafa kata ya Nyang’hwale, Pira Robert amesema makazi wanayoishi wananchi sio salama kwa kuwa ni maeneo ya milima ambako ndiko makazi ya fisi.

Robert aliwataka wananchi waliohamia kwenye maeneo ya pembezoni na milima kuhama na kurudi kwenye makazi yenye watu wengi ili kunusuru maisha yao.

 

Advertisement