Guardiola aungana na Aguero kuhusu kibendera mwanamke

Saturday October 24 2020
kibenderapic

Manchester, United Kingdom (AFP).Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola kwa mara nyingine amemtetea Sergio Aguero, akisema "alijua nia yake" baada ya Gary Neville kumshauri mshambuliaji huyo aombe radhi kwa kuweka mkono wake begani wa mwamuzi msaidizi wa kike, Sian Massey-Ellis.

Ushindi wa City wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Arsenal ulifunikwa na tukio hilo lililotokea katika kipindi cha pili wakati Aguero alipopingana na mwamuzi msaidizi wa kike kuhusu uamuzi wa kurusha mpira uliotoka kwenda City.

Baada ya kubishana na Massey-Ellis, Aguero aliweka mkono wake kwa muda mfupi begani kwa mwamuzi huyo msaidizi wakati alipoanza kuondoka.

Mshambuliaji huyo nyota wa Argentina alikosolewa na wengi katika mitandao ya kijamii, na gwiji wa Manchester United na mchambuzi wa soka, Neville aliiambia CNN akisema: "Nadhani angefanya vizuri kama akiomba radhi."

Chini ya kanuni zilizotungwa mwaka 2016, wachezaji wanaweza kuonywa au kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumgusa mwamuzi kutegemeana na tukio, lakini Chama cha Soka kimeamua kutochukua hatua.

Baada ya kuangalia tena tukio hilo, Chama cha Soka kiliridhika kuwa waamuzi wa mchezo huo hawakuona kama kulikuwa na umuhimu wa kuchukua hatua yoyote.

Advertisement

Guardiola alimtetea muda mfupi baada ya mechi akisema  "(Aguero) ni mtu mzuri kuliko wote niliowahi kukutana nao maishani mwangu".

Alipoulizwa jana Ijumaa kama mshambuliaji huyo anawajibika kuomba radhi, bosi huyo wa City alisema: "Najua nia ya Sergio.

"Aliweka mikono yake kwa njia ya kawaida, kama anavyofanya mara kwa mara kwangu, nje na ndani ya uwanja, au wakati napomkumbatia anapobadilishwa na wakati mwingine humgusa refa pia."

Guardiola aliongeza: "Nadhani ilikuwa kawaida kwa sababu namjua vizuri Sergio, ambaye amekuwa wa aina yake, nyota katika soka duniani na ni mmoja wa watu wanyenyekevu na wazuri kuliko wote niliokutana nao.

"Kitu muhimu ni nia yake, na nia ilikuwa ni kuzungumza naye kwa njia ya kawaida.Na nina uhakika -- sikuzungumza na Sergio kuhusu hili -- kama mwamuzi msaidizi alijisikia vibaya, angeomba radhi bila ya tatizo."

Advertisement