Hakimu jela kwa rushwa ya Sh150, 000

Muktasari:

Hakimu huyo wa Mahakama ya mwanzo Magugu Wilayani Babati aliomba na kupokea rushwa ya Sh150, 000 kutoka kwa ndugu wa  washtakiwa watatu ili kuwaachia kwenye kesi iliyokuwa ikiwakabili

Babati.Hakimu wa Mahakama ya mwanzo Magugu Mkoani Manyara, Adeltus Rweyendera amehukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Babati kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini Sh1.5 milioni kwa kosa la kupokea rushwa ya Sh150, 000.

Hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Andrew Kuppa akisoma hukumu ya kesi hiyo namba 137/2020 mjini Babati, amesema mshtakiwa huyo aliomba na kupokea rushwa hiyo kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupokea rushwa namba 11/2007.

Amesema Rweyendera aliomba fedha hizo kutoka kwa wazazi naa ndugu wa washtakiwa watatu ambao walikuwa wana kesi namba 242/2020 ikiwa ni kishawishi cha kuwasaidia na kuwaachia.

Amesema kutokana na ushahidi uliotolewa ukiongozwa na mawakili wa Takukuru, Martin Makani na Evelin Onditi, usioacha shaka dhidi ya mshtakiwa huyo, mahakama imemkuta na hatia na kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 1985.

Mkuu wa Takukuru mkoani Manyara, Hole Joseph Makungu amedai kuwa walipokea taarifa kwa msiri kwamba hakimu huyo alitaka fedha hizo wachangishane wazazi na ndugu.

Makani amesema baada ya kupokea taarifa hiyo ofisi yao ilifanya uchunguzi wa kina na kubaini kuwa ni kweli kesi tajwa ipo katika mahakama ya mwanzo Magugu na ilikuwa inasikilizwa na hakimu Richard Rweyendera.

"Uchunguzi wetu pia ulibaini kuwa washtakiwa hao walikuwa watatu, hivyo hakimu huyo alitaka watoe Sh50, 000 kila mmoja," amesema Makungu.

Amesema baada ya kujiridhisha na ukweli huo, maofisa wa Takukuru waliaandaa mtego wa rushwa na kufanikiwa kumkamata na fedha hizo na kisha kumfikisha mahakamani.