Hakimu wa zamani mahakama ya mwanzo Magomeni kupandishwa kizimbani

Wednesday September 11 2019

 

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni leo Jumatano Septemba 11, 2019 itawafikisha mahakamani watuhumiwa watatu wa rushwa baada ya kukamilika kwa ushahidi dhidi yao.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Septemba 11, 2019 mkuu wa Takukuru mkoa wa Kinondoni, Theresia Mnjagira amemtaja mtuhumiwa wa kwanza kuwa ni aliyekuwa hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Magomeni na mkazi wa Kijitonyama, Omary Mohammed Abdallah.

Mnjagira amesema Abdallah alitenda kosa Februari 12, 2017 baada ya kumtaka mtoa taarifa wa Takukuru ampatie Sh1 milioni ili amsaidie kwenye kesi yake ya mirathi iliyokuwa mbele yake, jambo ambalo amesema ni kinyume cha sheria. Abdallah anadaiwa kupokea rushwa ya Sh703,000 kati ya fedha alizohitaji.

"Mlalamikaji alitoa taarifa Takukuru Mkoa wa Kinondoni Machi Mosi, 2017 uchunguzi ulifanyika na kubaini kuwa tuhuma hizo ni za kweli," amesema Mnjagira.

Pia, amesema wanamfikisha mahakamani mfanyabiashara na mkazi wa Kibamba, George Barongo (37) kwa kuomba na kupokea rushwa ya Sh498,000 kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, namba 11/2007.

Katika tukio jingine, Takukuru mkoani humo itamfikisha mahakamani,  Nerbert Malevu (33) mkazi wa Nyakasangwe, kata ya Wazo ambaye ndiyo katibu wa kamati ya upimaji wa viwanja katika mtaa wa Nyakasangwe kwa kosa la kuomba rushwa ya Sh2.5 milioni na kupokea Sh500,000.

Advertisement

"Mlalamikaji alitoa taarifa Takukuru mkoa wa Kinondoni Agosti 16, 2019 ambapo uchunguzi ulifanyika na kubaini kuwa tuhuma hizo ni za kweli."

"Tuliandaa mtego wa rushwa na kumkamata mtuhumiwa Agosti 20, 2019 katika eneo la Mwenge Lukani Pub baada ya kupokea Sh500,000," amesema mkuu huyo wa Takukuru.

Advertisement