Halima Mdee achukuliwa fomu kutetea nafasi ya uenyekiti Bawacha, yeye azungumza

Muktasari:

Shughuli ya uchukuaji fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema katika mabaraza ya vijana, wazee, wanawake na chama chenyewe ngazi ya taifa, ulianza Novemba 18, 2019 na kuhitimishwa Novemba 30, 2019.

Dar es salaam. Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee anatarajia kutetea nafasi yake ya Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha) baada ya wanawake kujitolea kumchukulia fomu.

Uchaguzi wa mabaraza ya Chadema ya wanawake, vijana na wazee utaanza Desemba 10 na kuhitimishwa Desemba 18,2019 kwa uchaguzi ngazi ya taifa.

Shughuli ya uchukuaji na urejeshaji fomu ya kuwania nafasi hizo unaendelea na utahitimishwa Novemba 30, 2019.

Akizungumza na Mwananchi jana Jumatano Novemba 27, 2019, Katibu wa baraza hilo, Grace Tendega alisema wanatarajia kuwa na orodha ya wagombea ifikapo Novemba 30, 2019 saa kumi jioni.

"Kwa sasa wagombea wanachukua fomu maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye mtandao na ofisi za kanda, hadi sasa taarifa niliyonayo ni Halima Mdee kuchukuliwa fomu ya kugombea nafasi ya mwenyekiti," amesema Tendega ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum

Alisema mtu anaporudisha baada ya kulipia na kuwasilisha risiti ndio anaweza kufahamika lakini kwa sasa wapo wanaoendelea kuchukua kwenye ofisi za kanda na kwenye mitandao.

Kwa upande wa Mdee alisema fomu hiyo ilichukuliwa Jumamosi iliyopita Novemba 23, 2019 na wanawake mbalimbali waliojitolea hivyo anategemea kuirudisha kesho Ijumaa Novemba 29,2019.

Mwananchi lilimtafuta Mdee kuhusu uamuzi wa wanawake hao ambapo alisema, "wapo wanawake wamejitolea kunichukulia fomu, nitaijaza na kuirudisha siku ya Ijumaa kama ratiba inavyoelekeza mwisho ni Jumamosi Novemba 30," amesema Mdee