Haya ndiyo maajabu ya shule ya Kibaha

Muktasari:

Shule ya Sekondari Kibaya mkoani Pwani ambayo kwenye matokeo ya mitihani ya kidato cha sita mwaka 2019 imeshika nafasi ya sita kitaifa, lakini imekuwa na ufaulu mzuri wa  wanafunzi wake kupata daraja la kwanza wengi zaidi huku kukiwa hakuna daraja la nne au sifuri.

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani ya Taifa (Necta) jana  lilitangaza matokeo ya mtihani ya kidato cha sita uliofanyika kati ya Mei 6 hadi 23 mwaka 2019 yanayoonyesha Shule ya Sekondari Kibaha mkoani Pwani imeshushwa kwa nafasi sita.

Katika matokeo ya mwaka  2018, Kibaha ilikuwa ya kwanza kitaifa lakini mwaka huu shule hiyo imeshuka hadi nafasi ya sita na Kisimiri iliyokuwa ya pili mwaka jana mwaka huu ikipanda na kuongoza kitaifa.

Licha ya Kibaha kushika nafasi ya sita kitaifa, lakini matokeo yake yamekuwa mazuri kati ya wanafunzi 172 waliofanya mitihani mwaka huu, waliopata daraja la kwanza ni 143, daraja la pili 26 na daraja la tatu wakiwa ni watatu huku kukiwa hakuna daraja la nne wala sifuri.

Mwaka 2018 wakati Kibaha ilipoongoza kitaifa, kati ya wanafunzi 121 waliofanya mtihani, waliopata daraja la kwanza walikuwa 101, daraja la pili 17, daraja la tatu watato na hakukuwa na daraja la nne wala sifuri.

Katika matokeo hayo ambayo Kisimiri imeongoza, ilikuwa na watahiniwa 60 mwaka huu ambapo 58 wamepata daraja la kwanza na wawili wamepata daraja la pili. Idadi ya watahiniwa wa Kisimiri ni zaidi ya mara mbili ya wale wa Kibaha.

Mwaka 2018, Kisimiri iliposhika nafasi ya pili na Kibaha ya kwanza, ilikuwa na watahiniwa 67 ambapo waliopata daraja la kwanza waliokuwa 51 na daraja la pili walikuwa 16. Idadi hii ni karibu ya mara mbili ya wale wa Kibaha.

 Mkuu wa Shule ya Kibaha, Chrisdom Ambilikile alisema siri ya mafanikio ni nidhamu waliyoijenga kwa wanafunzi.

“Kwa idadi hii ya daraja la kwanza Kibaha ndio tunaongoza hakuna shule nyingine yenye daraja la kwanza wengi namna hii,” alisema Ambilikile.

Amesema idadi kubwa ya wanafunzi wa kidato cha sita mwaka jana iliwafanya wapinzani wao kuwapita, na hivyo kutoka kuwa namba moja mpaka namba sita licha ya kuwa kuwepo kumi bora ni furaha kwao.