Huyu ndiye Profesa Lipumba wa CUF

Mkutano mkuu ulioandaliwa na CUF upande wa Profesa Ibrahim Lipumba umemalizika na kumbakiza kiongozi huyo madarakani kama mwenyekiti, huku ukiiweka pembeni kambi ya aliyekuwa Katibu mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.

Mbali na Profesa Lipumba, kikao cha baraza kuu la uongozi wa chama hicho, pia kimemteua Khalifa Suleiman Khalifa kuwa Katibu mkuu akisaidiwa na Naibu katibu mkuu Fakhi Suleiman Khatibu (Zanzibar) na Magdalena Sakaya (Bara).

Profesa Lipumba anashika uenyekiti kwa mara ya tano mfululizo tangu alipochaguliwa mara ya kwanza mwaka 1999 akimrithi Musobi Mageni aliyestaafu nafasi hiyo. Anashika nafasi hiyo huku chama kikiwa katika mpasuko mkubwa kati yake na Maalim Seif.

Mzozo kati ya viongozi hao wawili ulianza Agosti 2015, baada ya Profesa Lipumba kutangaza kujivua wadhifa wa uenyekiti wa chama hicho, akipinga ujio wa Edward Lowassa kugombea urais kupitia Chadema na kuviwakilisha vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambavyo ni CUF, Chadema, NCCR na NLD.

Profesa Lipumba alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Ukawa baada ya vyama husika kujitoa kwenye vikao vya Bunge maalumu la katiba jijini Dodoma, Aprili 2014. Baada ya vyama hivyo kujitoa na kuanza kujipanga kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015, swali kubwa lilikuwa ni nani ataviwakilisha vyama hivyo kugombea urais, ikizingatiwa kuwa Profesa Lipumba alikuwa ameshagombea mara nne kupitia CUF.

Baada ya Profesa Lipumba kujitoa, CUF chini ya Katibu mkuu, Maalim Seif ilimteua Julius Mtatiro (sasa amehamia CCM) kuwa mwenyekiti wa kamati ya uongozi. Chama hicho kilikwenda katika uchaguzi bila ya kuwa na mwenyekiti wa chama. Hata hivyo, kilipambana na kufanikiwa kupata wabunge 42 Zanzibar na Tanzania bara wakiwamo wa viti maalumu.

Jambo kubwa linalotajwa kuwa kosa kwa kambi ya Maalim Seif ni kutoitisha mkutano mkuu mapema ili kuziba pengo la Profesa Lipumba alipotangaza kukaa pembeni, hivyo kumpa mwanya wa kurejea kwenye nafasi yake akidai kuwa ilikuwa wazi.

Mkutano mkuu ulipoitishwa mwaka mmoja baadaye, Agosti 2016, Profesa Lipumba aliandika barua ya kurejea kwenye nafasi yake na kuhudhuria mkutanoni hatua iliyolalamikiwa na upande wa Maalim Seif.

Hatua hiyo ilisababisha mkutano huo uliotakiwa kufanya uchaguzi, kuvunjika kutokana na mvutano wa pande mbili.

Upande mmoja ulimuunga mkono Lipumba na mwingine wa Maalim Seif.

Siku chache baadaye Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa ilimtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa CUF, jambo lililoongeza ‘chumvi’ kwenye mgogoro huo. Ofisi hiyo ilisimama bega kwa bega na Pofesa Lipumba hadi kwenye mkutano uliomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Alikotoka Profesa Lipumba

Licha ya kuwa mwanachama wa CCM tangu awali, Pofesa Lipumba aliamua kujiingiza kwenye siasa za wazi miaka michache baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi kwa kujiunga na CUF.

Profesa Lipumba alianza mbio za urais katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi nchini mwaka 1995 kupitia CUF na kuibuka nafasi ya tatu kwa asilimia 6.43, akiwa nyuma ya mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa (asilimia 61.82) na Augustine Mrema wa NCCR (27.77).

Mwaka 2000, aligombea urais kwa mara ya pili na kushika nafasi ya pili akipata asilimia 16.26 ya kura zote. Kwa mara nyingine mgombea wa CCM, Rais mstaafu Mkapa aliibuka mshindi kwa kupata asilimia 71.74 ya kura zilizopigwa.

Mwaka 2005, CUF ilimpa tena jukumu hilo kwa mara ya tatu, alipambana vikali na mwanasiasa maarufu wakati huo, Jakaya Kikwete wa CCM na kushika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 11.68. Kikwete alipata asilimia 80.28.

Profesa Lipumba aliwania tena kiti hicho mwaka 2010 kwa mara ya nne, safari hii aliibuka mshindi wa tatu kwa kupata asilimia 8.28 nyuma ya Rais mstaafu Kikwete aliyepata asilimia 62.83 na Dk Willibrod Slaa wa Chadema aliyepata asilimia 27.05.

Akimzungumza katika maandiko yake kupitia Gazeti la Mwananchi mwaka 2015, Julius Mtatiro ambaye sasa ni kada wa CCM, anasema Profesa Lipumba ni mtu mwenye heshima kubwa ndani na nje ya nchi kwa uchapakazi na misimamo yake katika ukuzaji wa uchumi.

“Si mtu wa kupenda kutumia umaarufu wake kufanya ‘siasa rahisi’ (cheap politics). Anaamini kuwa siasa si ujanjaujanja wala jambo la masihara,” anasema Mtatiro.

Pia, anataja suala la uadilifu na uwazi akisema, Profesa Lipumba si mtu wa kuingilia masuala ya fedha na hayamhusu kabisa, pia anachukia mbinu zozote zile zinazoweza kufanywa ndani ya chama chake na hata nje, zitakazoleta taswira ya kukosa uaminifu kwenye fedha.

Pia, Mtatiro anamtaja Profesa Lipumba kuwa na sifa ya kuishi maisha ya kawaida na ni mtu wa kujitolea katika jamii.

Mtatiro anamtaja Profesa Lipumba kuwa mtu wa kuchukulia kila jambo kitaaluma, akisema inamfanya wakati mwingine asieleweke kwa watu wanaomsikiliza hasa wasio na elimu kubwa. Mbali na hilo, anasema Profesa Lipumba ameacha mambo mengi yaamuliwe kwa mawazo, maoni na ushauri wa watu waliomzunguka kuliko kufanya uamuzi mgumu wakati akiwa mwenyekiti.

Baada ya kutengana na Maalim Seif

Licha ya sifa alizonazo kielimu na kazi zake, Profesa Lipumba hajaonyesha upinzani mkali mbele ya CCM kwa upande wa bara, huku akibebwa zaidi na matokeo ya Zanzibar ambako CUF imekuwa ikileta upinzani mkali tangu kwenye matokeo ya urais, wabunge na wawakilishi.

Katika chaguzi zote alizogombea urais mara nne mfululizo, licha ya kushindwa kwa mbali dhidi ya CCM, hakuwahi kupata zaidi ya wabunge wawili bara. Ni mwaka 2015 tu, ndipo CUF ilipopata wabunge 10 bara jambo linalowafanya baadhi ya watu waamini kuwa huenda walipatikana kutokana na nguvu ya ushawishi wa Lowassa aliyewakilisha vyama vya Ukawa.

Swali ambalo wengi wanajiuliza ni je, Profesa Lipumba ataibakisha au kuipandisha CUF kwa kuanza na uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu kisha Uchaguzi Mkuu wa mwakani ili kupata idadi kubwa ya wenyeviti wa mvitongoji, vijiji, mitaa, madiwani, wawakilishi, wabunge na pengine kunyakua urais 2020?