Magufuli: Uongozi ni pamoja na kuchafuliwa

Monday October 21 2019

 

By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baada ya kumaliza ziara ya mikoa ya Kusini katikati ya wiki iliyopita, Rais John Magufuli jana aliwaapisha viongozi wapya aliowateua huku akiwapa ujumbe kuwa ‘kazi ya uongozi ni pamoja na kuwatetea wananchi wanaowaongoza, lakini pia kusemwa vibaya na kuchafuliwa na baadhi ya watu’.

Rais alisema hayo dakika chache baada ya kuwaapisha Mathias Kabunduguru kuwa mtendaji mkuu wa Mahakama Tanzania, Godfrey Mweli kuwa naibu katibu mkuu wa Ofisa ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Ali Sakila kuwa balozi.

Wateule hao watatu ni miongoni mwa viongozi mbalimbali walioteuliwa na Rais Magufuli juzi kabla ya kuapishwa jana Ikulu jijini Dar es Salaam.

Matangazo ya moja kwa moja kupitia tovuti ya Ikulu yalionyesha kabla Rais hajaanza kuifanya shughuli ya kuapisha, waalikwa walikuwa wametulia kwenye viti vyao kwa takriban dakika 40 wakimsubiri aingie. Muda wote huo waalikwa walikuwa wakiburudika kwa nyimbo mbalimbali kutoka kwenye spika zilizokuwa ukumbini humo huku wimbo wa Injili unaoitwa‘Hauwezi Kushindana’ wa Goodluck Gozebert ukitawala.

Baada ya Rais Magufuli kumaliza kuapisha wateule hao na kuzungumza, bado wimbo huo uliendelea kutumika kama kibwagizo.

Akihutubia baada ya kuwaapisha wateule hao wapya, Rais Magufuli akiongea kwa utulivu, alisema “sisi kama viongozi tuna jukumu la kuwatetea hawa wananchi wanyonge... saa nyingine katika kazi hizi za uongozi zinahitaji uvumilivu na zinahitaji Mungu kumtanguliza mbele. Utasemwa saa nyingine, usisemwe vizuri, lakini hiyo ndiyo kazi ya uongozi. Kazi ya uongozi ni pamoja na kuchafuliwa.”

Advertisement

Aliwataka viongozi hao wamtangulize Mungu katika utendaji wao wa kazi kwenye maeneo waliyopangiwa.

Pia aliwapongeza kwa uteuzi na kuwataka kwenda kufanya kazi kwa kufuata sheria, kutimiza wajibu na haki ili kuwatumikia wananchi. “Naibu katibu mkuu Tamisemi, ukaangalie maslahi ya walimu hakuna sababu ya walimu kulalamika, kashirikiane na waziri kuisimamia wizara hii.

“Kashughulikie madai ya walimu, haiwezekani walimu na watumishi wengine hawapati stahiki zao na wewe upo kwa hiyo kashirikiane na watendaji wengine, tena ufanye kazi zaidi. Mimi nataka kazi zifanyike,” aliongeza Rais Magufuli, ambaye hivi karibuni alifanya ziara ya mikoa ya kusini ya Lindi na Mtwara na kukumbana na changamoto kadhaa.

Rais Magufuli amewahakikishia wakulima wa mkoa wa Lindi ambao wanalalamikia kudhulumiwa na viongozi wa vyama vya ushirika mkoani humo (Amcos) kiasi cha Sh1.2 bilioni na kuahidi kuwa watalipwa fedha zote baada ya viongozi 92 kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kueleza tayari Sh255 milioni zimerejeshwa.

“Mkumbuke miiko yenu ili mkayatimize majukumu yenu kwa ajili ya Watanzania, mkafanye kazi bila kumuonea mtu kwa kadri Mungu atakavyowabariki,” alisema Magufuli.

Pa alimtaka mtendaji mkuu mpya wa Mahakama, Kabunduguru kuendeleza kazi nzuri zifanywazo na mahakama kwa kushirikiana na watumishi wengine wa idara hiyo.

Magufuli pia alimpongeza mtendaji aliyepita wa idara hiyo, Hussein Katanga kwa kazi nzuri na kudokeza kuwa amepanga kumpa kazi ya ubalozi ili kumsaidia katika nchi ambayo hakuitaja.

Advertisement