Kampeni kupambana na malaria yazinduliwa

Friday November 8 2019

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini, Ummy Mwalimu akiwa na viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ‘Ziro Malaria’ ikiwa ni siku ya malaria kwa nchi za Sadc iliyoadhimishwa Kibaha mkoa wa Pwani leo. Picha na Ericky Boniphace 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Kibaha. Kampeni maalum ya kupambana na ugonjwa wa malaria imezinduliwa katika maadhimisho ya siku ya malaria ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) yaliyofanyika Kibaha nchini Tanzania.

Tanzania inakuwa nchi ya 11 kuzindua kampeni hiyo endelevu lengo likiwa kusaidia jitihada za kupunguza, kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030.

Akizindua kampeni hizo leo Ijumaa Novemba 8, 2019 mkoani Pwani mwenyekiti wa mawaziri wa sekta ya afya na Ukimwi wa nchi 16 za Sadc, Ummy Mwalimu amesema kampeni hiyo inalenga kuuweka ugonjwa huo kama ajenda katika maeneo yote ili kufanikisha malengo yaliyowekwa.

Ummy amesema takwimu zinaonyesha kiwango cha upuliziaji dawa ukoko na matumizi ya vyandarua vyenye dawa yamefikia asilimia 80 huku idadi ya vifo vitokanavyo na malaria vimepungua kufikia asilimia 39 kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2018.

“Idadi kubwa ya watu walio hatarini kupata malaria inaongezeka wakati huohuo imeelezwa kuwa asilimia 83 waliopo kwenye hatari ya kupata malaria wapo nchi za Sadc,” amesema.

Waziri Ummy amesema Tanzania imefanikiwa kupunguza malaria kati ya nchi wanachama, ni wakati sasa wa kujipanga ili kutokomeza kabisa ugonjwa huo.

Advertisement

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Ernest Ndikilo amesema katika Mkoa huo  maambukizi ya malaria yameshuka kwa asilimia 50 kwa kipindi cha mwaka 2015/2019.

“Tulichokifanya ni kupima na kutibu wagonjwa, kuwapa wajawazito tiba kinga, vyandarua vilivyowekwa dawa, na upuliziaji wa viuadudu umesaidia kupunguza malaria katika Mkoa wa Pwani,” amesema Ndikilo.

Advertisement