Kampeni za Lissu sasa ni anga kwa anga

Muktasari:

Mgombea Urais wa Chadema, Tundu Lissu ameanza kutumia chopa kukamilisha mikutano yake ya kampeni kwa siku 10 zilizobakia.

Babati. Mgombea urais wa Chadema, Tundu ameanza kutumia chopa kwenye kampeni zake za uchaguzi zikiwa zimebaki siku 10 kufikia siku ya uchaguzi mkuu, Oktoba 28.

Meneja kampeni wa Chadema, Amani Golugwa ametangaza hatua hiyo leo Jumapili Oktoba 28 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Wilayani Babati mkoani Manyara.

Mgombea huyo ameanza kutumia usafiri huo leo kwenda kuhutubia mikutano ya  Kateshi, Dareda, Mbulu na Karatu mjini.

“Mgombea wetu atakwenda kwenye mikutano mingine kwa chopa, tunaamini tutayafikia maeneo yote ndani ya siku 10 zilizobaki,” amesema Golugwa.

Itakumbukwa mgombea huyo alishindwa kutumia chopa hiyo mwanzoni mwa kampeni zake kwa kile Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ilichoeleza kuwa rubani aliyetakiwa kumwendesha alikuwa na umri mkubwa, jambo ambalo haliruhusiwi.

 

Akizungumza kwenye mkutano wa Babati, Lissu amesema wako tayari kupiga kura katika mazingira magumu waliyonayo na kushinda uchaguzi huu.

“Zikiwa zimebaki siku 10, tutapiga kura katika mazingira haya yasiyo ya haki na tutashinda uchaguzi huu,” amesema Lissu.