Lipumba amfananisha Maalim Seif na Lowassa

Muktasari:

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema hashangai Edward Lowassa kurudi CCM kwa sababu alikwenda upinzani kutafuta urais, lakini baada ya kuukosa amerudi kwenye chama chake.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amemfananisha katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwamba wote ni wabinafsi na wanatafuta urais kwa nguvu.

Profesa Lipumba ameyasema hayo leo Machi 6, 2019 wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuzungumzia suala la Lowassa kuhamia CCM na maandalizi ya chama chake kuandaa mkutano mkuu wa dharura.

Amesema wanasiasa hao wanafanana kwa sababu wote walijiunga na upinzani baada ya kukosa nafasi za kugombea urais wakiwa CCM.

Profesa Lipumba amesema pia hakukubaliana na uamuzi wa washirika wenzake kumchagua Lowassa kuwa mgombea urais wa Ukawa mwaka 2015.

Amesema aliamua kujitoa Ukawa kwa sababu hakukubaliana na utaratibu uliotumika kumchagua Lowassa na kwamba baada ya muda mfupi naye alitangaza nia ya kugombea urais, uamuzi ambao uliwaudhi wenzake wa Ukawa.

"Nijikute kweli Lipumba mimi nasimama jukwaani namnadi Lowassa? Japo wanasema mzigo mzito mpe Mnywamwezi, mgizo ule ulikuwa mzito sana," amesema Profesa Lipumba.

Mwanasiasa huyo amesema Maalim Seif naye aliingia upinzani baada ya kukosa fursa ya kugombea urais akiwa CCM.

Amesema kwamba hata ndani ya CUF, Maalim Seif amekuwa akiutaka urais kwa nguvu na kusahau malengo mengine ya kitaifa ya chama, jambo ambalo amesema lingekiwezesha chama hicho kuunda Serikali ya Zanzibar.

"Tunajifunza kama vyama, lazima tuwe na malengo ya kitaifa ya chama. Tungepeleka kesi mahakamani baada ya uchaguzi, leo tungekuwa na Serikali ya umoja wa kitaifa, lakini kwa sababu ya ubinafsi wa Maalim Seif kuutaka urais, kesi haikufunguliwa.”

Kwa sasa CUF imegawanyika katika pande mbili ukiwamo upande unaomuunga mkono Profesa Lipumba na ule wa Maalim Seif. Pande hizo ziliibuka baada ya kurejea kwa Lipumba ndani ya chama hicho kufuatia awali kujiondoa.