VIDEO: Lipumba amuangukia Magufuli

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (kushoto) akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, kuhusu changamoto walizokutananazo wagombea wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa chama hicho. Kulia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazee wa chama hicho, Mohamed Chunga na katikati ni Mkurugenzi wa Uchaguzi na Itifaki, Mohamed Masoud. Picha na Said Khamis

Dar/ mikoani. Kila kona ni vilio. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na malalamiko ya vyama vya upinzani kuhusu mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24.

Wakati vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi na TLP vikilalamika ukiukwaji wa kanuni na kufanyiwa hujuma zilizosababisha kuenguliwa kwa wagombea wao wengi kwenye mchakato wa uchaguzi huo, hali ni tofauti kwa CCM. Chama tawala wanashangilia ushindi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa maeneo mbalimbali nchini kwa wagombea wake kutangazwa kupita bila kupingwa.

Bungeni mjini Dodoma wabunge wa Chadema na CUF waliomba mwongozo wakitaka Bunge kusitisha shughuli zake ili kujadili sintofahamu ya uchaguzi huo, lakini Naibu Spika, Dk Tulia Ackson aliwafahamisha kuwa tayari Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo ameshatoa maelezo ya kasoro hizo kutaka zifanyiwe kazi.

Nafasi zinazowaniwa katika uchaguzi huo ni mwenyekiti wa kitongoji, mwenyekiti wa kijiji, mwenyekiti wa mtaa, wajumbe wa halmashauri ya kijiji na wajumbe wa kamati ya mtaa.

Jana, NCCR-Mageuzi imetangaza kwenda mahakamani kupinga utaratibu uliotumika katika uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uchaguzi huo huku mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akimuomba Rais John Magufuli kuingilia kati akitaja kasoro tatu.

Katibu mwenezi wa NCCR-Mageuzi, Hemed Msabaha alisema kitendo cha wasimamizi wa uchaguzi kufunga vituo katika baadhi ya maeneo hususan Jimbo la Vunjo kwa siku nne ni ukiukaji wa kanuni.

“Tumeamua kufanya mambo mawili. Tumewaelekeza wale walioenguliwa wakate rufaa kikanuni, pili tunakwenda mahakamani kupinga utaratibu wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu,” alisema.

Msabaha alisema kanuni ya 17(2) ya kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 inataka vituo vifunguliwe saa 1:30 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.

“Kifungu cha 17(3) kinasema zoezi la uchukuaji na urudishaji wa fomu litakuwa ndani ya wiki moja. Sasa kwenye Jimbo la Vunjo kwa mfano zoezi hilo limefanyika kwa siku tatu tu kinyume cha kanuni.”

Ni kutokana na hilo, alisema NCCR-Mageuzi imeanzisha mchakato wa kufungua kesi mahakamani, ili mamlaka iliyohusika kusimamia uchaguzi huo iweze kuwajibishwa kwa ubatili aliodai wameufanya.

“Kwa wale wenye fomu mkononi baada ya vituo kufungwa siku nne mfululizo tumewataka wawe wapole wakati tukikamilisha taratibu za kwenda mahakamani kudai haki yetu,” alisisitiza Msabaha.

Akizungumza,Profesa Lipumba jana alisema Tamisemi iliyo katika ofisi ya Rais inahusika moja kwa moja na mambo yanayotokea katika uchaguzi huo. “Ili kuepusha uvunjifu wa amani ni vyema Rais Magufuli kuingilia kati na kuongeza siku nne za uchukuaji fomu na ofisi zote ziwe wazi ili walionyimwa fursa waweze kuchukua, kujaza na kurejesha,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema jambo la pili kila aliyechukua fomu na kudhaminiwa na chama cha siasa ateuliwe kugombea.

“Wapo baadhi ya wananchi na wagombea walioondolewa katika daftari la wakazi nao warejeshwe ili waweze kutekeleza haki yao ya kikatiba,” alisema Profesa Lipumba. Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema alisema kilichofanyika katika mchakato wa uchaguzi huo hasa Jimbo la Vunjo ni mkakati aliodai ni mbaya na hauna dhamira njema. “Ni mkakati mbaya sana na usipodhibitiwa nina wasiwasi mwaka 2020 watamfanyia tena Rais wetu,” alisema Mrema na kusisitiza kuwa haamini hayo yaliyofanyika yana mkono wa Rais.

“Ni mkakati uliotengenezwa kwanza ili kuonyesha serikali iliyo madarakani utawala wake hauzingatii haki na hauzingatii sheria. Sidhani kama ni Rais aliwatuma. Nasema hivyo kwa sababu pamoja na maneno mazuri ya Jafo (Seleman- Waziri wa Tamisemi) kuwa tukate rufaa unakata rufaa kwa lipi na unamkatia nani wakati huku kwangu tulinyimwa hadi fomu za kugombea,” alisema Mrema.

Mkoani Mwanza msimamizi wa uchaguzi halmashauri ya wilaya ya Tarime, Peter Nyanja aliwaagiza wasimamizi wasaidizi kutotumia makosa madogo ikiwemo kukosea sarufi kuwaengua wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.