Lissu: Sitaficha tarehe ya kurejea Tanzania

Muktasari:

Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu  amesema atarejea Tanzania kutoka nchini Ubelgiji anakoendelea na utaratibu, akisisitiza kuwa jambo hilo halitakuwa siri kama ambavyo anaombwa na watu wengi, “Nitarejea Tanzania mchana kweupe, sina sababu ya kuficha.”

Dar es Salaam. Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu  amerudia tena ahadi yake kuwa atarejea Tanzania “mchana kweupe” akitokea Ubelgiji alikoenda kutibiwa, akisema suala hilo halitakuwa siri kama ambavyo anashauriwa na watu wengi.

“Nitarejea Tanzania mchana kweupe, sina sababu ya kuficha,” amesema Lissu katika andiko lake la simulizi ya mkasa wake aliloandika jana Septemba 7, ikiwa ni miaka miwili kamili tangu aliposhambuliwa kwa risasi akiwa Dodoma.

Katika andiko hilo lenye kichwa cha habari kisemacho “Miaka Miwili ya Mateso, Matumaini”, Lissu amewashukuru waliomsaidia, mateso aliyopitia na suala la kurejea Tanzania.

Amesema licha ya kushauriwa na watu afanye siri siku ya kurejea nchini, haoni umuhimu wa kufanya hivyo kwa kuwa si mhalifu.

Hata hivyo, siku tano zilizopita katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC), Lissu aliahirisha uamuzi wake wa kurejea Septemba 7, 2019 kama alivyoahidi awali, akisema bado hajapata ruhusa ya madaktari wake wanaotaka kuonana naye Oktoba, 2019.

Lissu alishambuliwa kwa risasi akiwa kwenye gari nje ya makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge na jana ilikuwa siku ya kumbukumbu ya miaka miwili tangu tukio hilo litokee saa 7:00 mchana siku hiyo.

Baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kisha usiku alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako alitibiwa hadi Januari 6, 2018 alipopelekwa nchini Ubelgiji kukamilisha matibabu na hadi sasa yuko aktika taifa hilo la barani Ulaya.

 “Nimeshauriana na ninaendelea kushauriana na viongozi wenzangu wa chama, pamoja na familia yangu kuhusu tarehe muafaka ya kurudi nyumbani,” anasema Lissu.

 “Nimezungumza pia na ninaendelea kuzungumza na viongozi mbalimbali wa kisiasa, kidini na wa taasisi za kijamii nchini kwetu.

“Nimezungumza na ninaendelea kuzungumza na wawakilishi wa nchi marafiki wa Tanzania, mashirika na taasisi za kimataifa na za kikanda na mashirika ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu.”

Amesema lengo la mazungumzo na mashauriano hayo  ni kuhakikisha mazingira salama na muafaka ya kurudi nchini.

“Baada ya mashauriano yote haya, tutakubaliana kuhusu siku na utaratibu mzuri na salama zaidi wa kurudi kwangu nyumbani. Siku na utaratibu tutakaokubaliana utatoa muda wa kutosha kufanya maandalizi yote yanayohitajika, ndani na nje ya Tanzania. Siku na utaratibu huo utatangazwa kwa umma katika muda muafaka,” amesema Lissu.

Amesema kwa kuelewa tukio lililompata, baadhi ya watu wamemshauri tarehe ya kurejea iwe siri.

“Pamoja na hiyo nia njema, siafikiani na ushauri huu. Mimi si mhalifu kwa hiyo siwezi kurudi nyumbani kwetu kwa kificho. Badala yake nitarudi nyumbani kwetu mchana kweupe mbele ya macho ya Watanzania na ya dunia nzima,” ameandika mwanasheria huyo.

Serikali ndio yenye wajibu wa kisheria wa kuhakikisha ulinzi na usalama wangu nitakaporudi nyumbani. Kwa sababu hiyo hatuwezi na haitakuwa busara kuifanya tarehe ya kurudi kwangu kuwa siri.”

Amesema Watanzania wengi ambao wamemuombea na kumchangia fedha na rasilimali zilizomuwezesha kuishi na kupata matibabu Kenya na Ubelgiji, wangependa kwenda uwanja wa ndege kumpokea.

“Mimi mwenyewe ningependa kupokelewa na watu wengi iwezekanavyo baada ya yote ambayo nimepitia na ambayo nchi yetu imepitia  tangu Septemba 7, 2017,” amesema Lissu.

Amesema vyombo vya habari vya Tanzania na vya kimataifa,  marafiki wa Tanzania katika jumuiya ya kimataifa wangependa kujua siku na tarehe ya kurudi kwake ili waweze kufuatilia tukio hilo kwa ukaribu zaidi.

“Kuna wawakilishi wa taasisi za kidini na kijamii, ndani na nje ya nchi yetu, wanadiplomasia kutoka nchi rafiki na mashirika ya kimataifa, pamoja na wawakilishi wa vyombo vya habari vya kimataifa ambao wameonyesha nia ya kunisindikiza katika safari yangu ya kurudi nyumbani,” amesema Lissu.