Lugola azungumzia Chadema kujitoa kushiriki uchaguzi Serikali za mitaa

Muktasari:

  • Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania,  Kangi Lugola amedai chama cha siasa kilichojitoa kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 kinapanga kufanya vurugu.

Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania,  Kangi Lugola amedai chama cha siasa kilichojitoa kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 kinapanga kufanya vurugu.

Jana Alhamisi Novemba 7, 2019 mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza chama hicho kujitoa kushiriki uchaguzi huo kutokana na wagombea wake wengi kuenguliwa pamoja na ukiukwaji wa kanuni na taratibu.

Lugola ameeleza hayo leo Ijumaa Novemba 8, 2019 bungeni mjini Dodoma wakati akijibu mwongo wa wabunge wa CCM, Godluck Mlinga (Ulanga) na Richard Ndasa (Sumve) waliohoji sababu Chadema kujitoa katika uchaguzi.

Goodluck Mlinga aliomba mwongozo na kuhusisha  uamuzi wa Chadema kujitoa kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa, na vurugu zinazojitokeza.

Mbunge huyo amesema Chadema kimekuwa kikisusa kushiriki chaguzi mbalimbali na akataka kujua hatua ambazo Serikali itazichukua dhidi ya chama hicho. Mwongozo kama huo pia uliombwa na mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa.

Akijibu miongozo hiyo baada ya kupewa nafasi na mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, Waziri huyo wa Mambo ya Ndani amesema Serikali haitanyamaza wala kutochukua hatua kwa vitendo vinavyohatarisha usalama na mali za wananchi.

Amesema polisi wamejipanga kuchukua hatua kwa mtu yeyote, vikundi ama vyama vya siasa  vitakavyofanya fujo wakati wote wa mchakato wa uchaguzi wa Serikali za mitaa.

“Nina taarifa chama kimoja kimejitoa katika uchaguzi ni imani yangu kuwa chama hiki kinaweza kikawa na mpango wa kufanya fujo ya kuvuruga amani na usalama wa nchi hii,” amesema Lugola.

Amesema hakutakuwa na nafasi yoyote ya vyama vya siasa kufanya mipango inayovunja na kuhatarisha imani ya nchi.