Maendeleo ya Watanzania yamerudi nyuma-Ripoti UNDP

Dar es Salaam. Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu ya mwaka 2019 inaonyesha kwa ujumla maendeleo ya binadamu nchini kwa mwaka 2018 yalirudi nyuma kwa asilimia 24.9, ikilinganishwa na mwaka 2017.

Uchambuzi katika ripoti hiyo umezingatia hali ya kutokuwapo usawa katika mazingira ya kuzaliwa mtoto, katika kipato, katika elimu na katika tofauti kwa wenye mali na wasiokuwa nazo.

Pamoja na hali hiyo, Tanzania bado inaonekana kuwa juu ya makadirio ya jumla katika ukanda wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara (asilimia 30.5) na kidunia (asilimia 31.1).

Ripoti hiyo ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) iliyozinduliwa Desemba 18, mwaka jana ikiwa na jina la “Mtizamo wa Zaidi ya Pato, Zaidi ya Wastani, Zaidi ya Mahitaji ya Leo: Tofauti za Kijamii na Kiuchuni Katika Karne ya 21”, inahusisha nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN).

“Maendeleo yamerudi nyuma kutokana na ukuaji wa uchumi kutokuwa jumuishi katika sekta zinazohusisha maisha ya Watanzania wengi,” alisema Dk Abel Kinyondo wa Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Katika miongo miwili iliyopita, uchumi umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 7, lakini unahusisha sekta zisizokuwa na ajira ya Watanzania wengi. Ndio maana unasikia wanalalamika uchumi unakuwaje wakati hakuna pesa. Matokeo yake tabaka la maskini na tajiri linaongezeka.

“Kwa mfano, kuanzia mwaka 2016 hadi sasa kulikuwa na madai ya nyongeza za mishahara, ajira , kutopandishwa vyeo. Maana yake ni kwamba purchasing power (uwezo wa kifedha) inashuka kwao, kwa hiyo pengo linaongezeka la kutokuwapo na usawa katika maeneo hayo.”

Hata hivyo, Humphrey Moshi wa Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anatofautiana na maoni ya Dk Kinyondo.

“Takwimu zinakinzana na uhalisia unaoendelea katika uwekezaji katika sekta ya elimu, pamoja na huduma mbalimbali za kijamii,” alisema.

Lakini alikubaliana na kuongezeka kwa tofauti katika jamii duniani, akisema inatokana na utandawazi.

“Na hali inaonyesha tofauti hiyo inaweza kuongezeka zaidi katika tofauti za kijamii,” alisema.

Ripoti hiyo pia inaitaja Tanzania kudondoka katika viashiria vya maendeleo ya binadamu kwa mwaka 2018 baada ya kupata alama 0.528 ikilinganishwa na alama 0.519 ilizopata mwaka 2015. Licha ya kuwa juu ya wastani wa kikanda na kidunia. Tanzania imeshika nafasi ya 159 kati ya nchi 189.

“Kwa mwaka 2018, Tanzania ilipata alama 0.528. Hata hivyo baada ya viashiria kutazamwa kwa jicho la usawa, viashiria vilishuka kwa Tanzania hadi asilimia 0.397,” inasema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inasema endapo jamii zikiondoa mwanya katika usawa wa kijinsia katika shughuli za kilimo, huenda uzalishaji ukaongezeka kutoka asilimia 7 hadi asilimia 19, ikizitaja Tanzania, Malawi na Rwanda.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa alisema maendeleo ya watu yanatakiwa kwenda sambamba na maendeleo ya vitu.

“Maendeleo ni sehemu ya haki za binadamu kwa hiyo ni vyema Serikali ikakumbuka kuweka uwiano sawa katika maendeleo ya watu na vitu,” alisema.

Maji bado vijijini

Ripoti hiyo inaonyesha asilimia 85 ya watu waishio mijini nchini ndiyo wanapata huduma za maji safi na salama huku vijijini wakiwa ni takribani asilimia 43 tu.

Takwimu hizo hazijatofautiana kwa kiwango kikubwa na za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kwa mujibu wa katibu mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo.

Kitila alisema takwimu za mwaka 2015/2016 zinaonyesha asilimia 47 ya Watanzania ndio wanapata maji safi na salama vijijini.

“Kwa takwimu za NBS za Desemba mwaka jana, kuna asilimia 64.8 vijijini, kazi inafanyika lakini bado tunatakiwa kuongeza kasi zaidi vijijini. Kazi hii inachagizwa na uanzishwaji wa wakala wa huduma za maji vijijini,” alisema Profesa Kitila.

Hata hivyo, Januari mwaka jana, Profesa Kitila alinukuliwa akisema ukosefu wa weledi kwa wahandisi umesababisha kukwama kwa miradi ya maji vijijini.

Matokeo mengine

Kwa mwaka 2018, tofauti ya kipato kwa Watanzania ilikuwa ni asilimia 22.4, juu ya wastani wa asilimia 27.6 ambayo ni makadirio ya nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara, na kidunia ni asilimia 25.

Hali ya kutokuwa na usawa katika umri wa kuishi imepata asilimia 25.3 juu ya malengo ya nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.

Akizungumza na Mwananchi jana, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile alisema bado hajaisoma ripoti hiyo hivyo alisema ataizungumzia baadaye.