VIDEO: Magufuli awapa fedha majeruhi 43, ataka watibiwe kwa gharama za Serikali

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania,  John Magufuli amewatembelea majeruhi 43 wa ajali ya moto iliyotokea jana mkoani Morogoro waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kuwapatia kila mmoja Sh500,000 kwa ajili ya matumizi mbalimbali

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania,  John Magufuli amewatembelea majeruhi 43 wa ajali ya moto iliyotokea jana mkoani Morogoro waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kuwapatia kila mmoja Sh500,000 kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Ajali hiyo ilitotokea jana Jumamosi Agosti 10, 2019 katika mtaa wa Itigi, Msamvu mkoani Morogoro mita 200 kabla ya kufika kituo cha mabasi cha Msamvu barabara ya Morogoro- Dar es Salaam baada ya lori la mafuta kupinduka na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta.

Majeruhi 46 waliokuwa wamelazwa katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro walihamishiwa MNH. Hata hivyo, watatu kati yao wamefariki dunia leo.

Akiwa katika wodi ya Sewahaji na Mwaisela, alizungumza na  majeruhi hao kuwashukuru wauguzi pamoja na madaktari kwa huduma nzuri na kuwazawadia  Sh1 milioni.

 “Watanzania tuendelee kuwaombea ndugu zetu hapa walipo wameungua ndani na nje kama alivyoleza daktari hii ina maana wana majeraha ya moto lakini pia walikuwa wanavuta hewa ya mafuta ya petroli,” amesema Magufuli.

Amewaagiza  madaktari kuhudumia majeruhi hao na kuwapatia mahitaji yoyote wanayohitaji kwa gharama ya Serikali.

“Serikali italipa chochote  watakachohitaji, wapatiwe matibabu daraja la kwanza  endeleeni kuwahudumia na mumtangulize Mungu mbele lakini pia Watanzania kila mmoja katika imani yake waombeeni wenzetu wameumia sana wanapata mateso,” amesema.

Akizungumza mara baada ya kupokea kiasi hicho cha fedha mmoja wa majeruhi, Rajabu Ally alimshukuru Rais kwa kumfariji na baada ya kuulizwa kuhusu ajali hiyo amesema, “Mimi nashukuru Mungu nimenusurika sikujua hata kilichotokea niliona tu moto unanifuata.”

Majeruhi mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Asha, mama lishe katika stendi ya mabasi ya Msamvu amemshukuru Magufuli na kubainisha kuwa hakujua kilichotokea.