Magufuli azungumzia ugumu anaokutana nao katika kuteua, kutengua

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli asema kazi ya kuteua na kutengua ni kazi yenye machungu, aeleza pia mkoa wa Morogoro ulivyowapa wakati mgumu kuuongoza.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema  kazi ya kuteua na kutengua viongozi mbalimbali ni kazi yenye machungu

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Septemba 22, 2019  Ikulu Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi wapya aliowateua akiwemo mkuu wa mkoa wa Morogoro, Loata Sanare na makatibu tawala na manaibu makatibu wa wakuu wa wizara mbalimbali.

Ijumaa iliyopita ya Septemba 20, 2019 Rais Magufuli alifanya uteuzi wa viongozi mbalimbali ikiwemo Sanare kuchukua nafasi ya Dk Stephen Kebwe ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Katika hafla hiyo baada ya kutoa salama kwa viongozi walioteuliwa Rais Magufuli amesema “Kiukweli kazi ya kuteua na kutengua ni ngumu sana. Kama kuna kazi inayonipa shida sana ni kumteua mtu kisha baadaye unamtengua.”

“Ni kazi ambayo ina machungu, lakini saa nyingine inabidi ufanye. Namshukuru Dk Kebwe yupo hapa, lakini ukweli bila unafiki kama kuna mkoa uliotusumbua katika kuongoza ni Morogoro,” amesema

Rais Magufuli amesema mambo mengi katika mkoa huo, hayakwenda na asiposema jambo ataonekana ni mnafiki na yeye hapendi kuwa hivyo.

Alitolea mfano katika halmashauri za mkoa huo kuwa  matumizi ya fedha ni ovyo na alishatuma Waziri wa Nchi, 0fisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo kufuatilia akabaini changamoto hizo huku ujenzi wa vituo vya afya havikamiliki wakati fedha zipo.

“Migororo ya ardhi haishi, kuna wawekezaji wa kiwanda cha Tumbuka wanataka kuondoka. Tulianza kuondoa wakurugenzi tulianza na wa Malinyi, tukadhani tumetibu kumbe hakuna, tukatoa wa halmashauri wa Morogoro Vijijini.”

“Aliyekuwa RAS wa mkoa ule nilimwambia katibu mkuu kiongozi amuelekeze astaafu, kwa sababu kazi yake ilikuwa ni kupanga walimu wa sekondari  na msingi kuwatoa vijijini na kuwaleta mjini. Ukishapewa na mahali umeaminika na Watanzania wote, halafu  walioko chini yako wanafanya mambo ya ovyo maana yake wewe hautoshi,” amesema