Mahakama Tanzania kufanya kazi kimtandao kuanzia 2020

Monday December 2 2019

Jaji Mkuu wa Tanzania profess Ibrahim Juma

Jaji Mkuu wa Tanzania profess Ibrahim Juma akifungua mafunzo ya majaji wafawidhi na baadhi ya majaji wa mahakama kuu nchini. 

By Mussa Juma, Mwananchi [email protected]

Arusha. Mahakama ya Tanzania kuanzia Januari 2020 zitaanza kutoa huduma kielektroniki ikiwapo kufungua kesi, kupata mwenendo wa kesi hadi hukumu ili kuongeza uwazi na kudhibiti uvunjifu wa maadili.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma ametoa taarifa hiyo, leo Jumatatu Desemba 2, 2019 wakati akifungua mafunzo ya majaji wafawidhi na majaji wa Mahakama Kuu wa Tanzania lenye lengo la kuboresha utendaji kazi kwa majaji hao.

Amesema Mahakama haziwezi kubaki nyuma na kujitenga na mahitaji makubwa ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) hivyo, kuanzia Januari itajikita katika matumizi hayo  ili kuongeza uwazi na kuondoa malalamiko ya kupotea majalada ya kesi na tarehe za kesi kutojulikana.

"Matumizi haya ya Tehama pia yatasaidia sana kupatikana  hukumu  za kesi kwa wakati na baada ya kufungua kesi unaweza kufuatilia kesi imekwama wapi na imekwama kwa nani," amesema

Amesema kwa kuanzia mahakama zote nchini isipokuwa mahakama ya mwanzo, zitaungwa katika mfumo wa Tehama wa Mahakama ili kurahisisha utendaji na ufuatiliaji wa kesi.

Jaji mkuu amesema kutokana na matumizi ya Tehama, watu ambao wamefungua kesi watakuwa na uwezo wa kulalamika kupitia simu zao za mikononi lakini pia kupata tarehe za kesi zao kupitia simu zao.

Advertisement

Awali,  Jaji Kiongozi, Eliezer  Felesh amesema lengo la maboresho ya utendaji wa ndani ya mahakama ni kuhakikisha huduma za utolewaji haki zinaboreshwa lakini pia zinatolewa kwa wakati.

"Kuna usemi wa kisheria kuwa haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa hivyo kwa maboresho ya utendaji wa mahakama hatutarajii haki kuendelea kucheleweshwa," amesema

Amesema katika mafunzo hayo ya majaji pia watapata  fursa ya kufanya tathimini ya utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitano wa mahakama ulianza mwaka 2015/16 hadi 2019/20 na kuja na vipaumbele vya mpango mkakati ujao

Advertisement