VIDEO: Mahakama yaelezwa mwandishi Erick Kabendera amepooza mguu mmoja na ana tatizo la kupumua

Muktasari:

Upande wa utetezi katika kesi inayomkabili mwandishi wa habari Erick Kabendera, wameiomba Mahakama  kulielekeza jeshi la magereza mteja wao kwenda kupatiwa vipimo hospitali ya serikali.

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mwandishi wa habari nchini Tanzania, Erick Kabendera, wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kulielekeza Jeshi la Magereza mteja wao kwenda kupimwa katika hospitali ya Serikali.

Wakili wa utetezi, Jebra Kambole amedai leo Ijumaa Agosti 30, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Mtega baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali Wankyo Saimon kueleza upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Wakili Kambole amedai usiku wa kuamkia Agosti 2, 2019 mteja wake akiwa gerezani alianza kuumwa na hadi leo ana shida ya kupumua.

"Nilienda kumuona nikakuta amepooza mguu na kushindwa kutembea kwa siku mbili pamoja na kuishiwa nguvu, sisi kama mawakili na ndugu hatujui nini anachoumwa."

"Kwa kuwa mteja wetu hajapata vipimo ambavyo vinastahili tunaomba Mahakama ielekeze Jeshi la Magereza mteja wetu akapimwe katika hospitali yoyote ya serikali ikiwemo Muhimbili penye vipimo vya uhakika," amedai Wakili Kambole

Wakili Wakyo amedai swala la ugonjwa hakuna mtu anayeweza kupingana nalo lakini huwezi kulielekeza Jeshi la Magereza kwenda kumpima katika hospitali fulani.

"Mahakama yako haiwezi kuamuru kupelekwa hospitali fulani kwa kuwa hajawahi kuwasilisha maombi akakataliwa lakini sheria inasema makosa ya uhujumu uchumi yanasikilizwa na Mahakama Kuu hivyo Mahakama hii haina uwezo wa kutoa uamuzi wowote" ameeleza Wakili Wankyo

Hakimu Mtega baada ya kusikiliza hoja za upande zote ameahirisha kesi hadi Septemba 12, 2019 itakapotajwa. Hata hivyo, hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi tarehe hiyo ambayo atakuwepo hakimu husika anayesikiliza kesi hiyo ambaye ni Agustino Rwizile

Kabendera amefikishwa  mahakamani kwa mara ya kwanza, Agosti 5, 2019 akikabiliwa na mashtaka matatu, ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kukwepa kodi na kutakatisha zaidi ya Sh173.2 milioni.

Mshtakiwa alisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustine Rwizile.

Katika kesi ya msingi,  mshtakiwa anadaiwa katika siku tofauti tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 2019 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Kabendera alitoa msaada katika genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

Katika shtaka la pili lililosomwa na wakili Wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi imedaiwa, siku na mahali hapo mshtakiwa bila kuwa na sababu za msingi kisheria alishindwa kulipa kodi ya Sh173, 247,047.02 ambayo ilitakiwa ilipwe kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)

Katika shtaka la utakatishaji fedha lililosomwa na Wankyo Simon  imedaiwa, kati ya Januari 2015 na Julai 2019 ndani ya jiji na mkoa wa Dar es Salaam mshtakiwa alijipatia kiasi hicho cha Sh173.2 milioni wakati akizipokea alijua kuwa fedha hizo ni mazao ya makosa tangulizi ya kukwepa Kodi na kujihusisha na genge la uhalifu.

Hata hivyo, mshtakiwa Kabendera hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa kwa kupata kibali kutoka kwa DPP.