Majaliwa asema tani 235,000 za pamba zimenunuliwa

Thursday September 12 2019Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema hadi juzi Jumanne Septemba 10, 2019 tani 235,000 za pamba zilikuwa zimenunuliwa na kuwahakikishia wafanyabiashara kwamba zilizobaki pia zitanunuliwa.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Septemba 12, 2019 wakati akijibu swali la Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndasa.

Mbunge huyo amehoji kauli ya Serikali kuhusu wakulima waliohifadhi pamba majumbani mwao bila kulipwa chochote.

Ndasa amesema katika msimu huu zao hilo limekumbana na kadhia mbalimbali na kuhoji kuhusu tani 35,000 zilizochukuliwa na wanunuzi na wakulima kukopwa pamoja na tani 52,000 zilizopo kwenye maghala kupitia chama cha ushiriki cha msingi (Amcos).

Ndasa amesema wakulima wamekopwa hawajalipwa na tani 70,000 zinakisiwa kuwa katika maghala, bado hazijapelekwa kwenye soko.

“Ningependa kujua nini kauli ya serikali au tamko la Serikali kuhusu wakulima wa zao la pamba ambao pamba  yao ipo nyumbani lakini wamekopwa hawajalipwa,” amehoji.

Advertisement

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema pamba na uzalishaji wake  umeongezeka kutoka tani 220,000 mwaka uliopita hadi tani 300,000  msimu huu na kwamba mwaka 2019 wanategemea kupata zaidi ya tani hizo.

Amesema Serikali imeendelea kupokea malalamiko ya wakulima kuhusu pamba kutonunuliwa.

Amebainisha kuwa wamekutana na wakaulima, wanunuzi, wafanyabiashara ili kuona namna ya kuiondoa pamba hiyo mikononi mwa wakulima.

“Nafurahi kusema utaratibu ambao tumeweka wiki tatu zilizopita umeanza kuleta matunda kwamba sasa wanunuzi wa pamba tumeshafikia asilimia kama 80 hivi kwa sababu mpaka juzi tumenunua tani 235,000, pamba ambayo ipo ni kidogo hivyo tunaamini kuwa tutachukua yote,” amesema.

Amewahakikishia  wakulima kwamba pamba hiyo itachukuliwa  baada ya kuchanganua iliyobaki kwao,  wameigawa kwa wanunuzi maalum ambao wana uhakika wa kuinunua.

Amesema kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT)  kupitia mabenki, wanunuzi hao wanapewa fedha na kwenda kuchukua pamba yote mikononi mwa wakulima, akibainisha kuwa zoezi la kuwapa fedha linaendelea na wanunuzi wanakwenda kuchukua pamba.

Amewahakikishia wakulima wa pamba kupitia wabunge kwenye mikoa yote nchini kuwa pamba yote itachukuliwa kwa sababu  mpango wa fedha kuwapatia wanunuzi upo.

Advertisement