Majaliwa ataka ma-DC kuwachukulia hatua watumishi wa umma wazembe

Saturday August 24 2019

 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa Wilaya nchini kuhakikisha wanawasimamia vyema watumishi wa umma na kuwachukulia hatua watakaobainika kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Majaliwa ametoa maagizo hayo jana Ijumaa Agosti 23, 2019 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Rutaba mkoani Lindi katika ziara ya kikazi.

Majaliwa amesema ni lazima kila mtumishi wa umma anayelipwa mshahara kwa kodi za wananchi ahakikishe anatekeleza ipasavyo majukumu yake kwa maelezo kuwa asipofanya hivyo hatakuwa na nafasi ya kuendelea kufanya kazi serikalini.

“Watumishi fanyeni kazi kwa bidii na msitarajie kuundiwa tume pale mnapofanya vibaya, ukiharibu kazi tunakushughulikia hapohapo na huu ndio msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano,” amesema.

Amesema watumishi wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni za kazi na pia watambue dhamana kubwa waliyonayo ambayo ni kuwahudumia wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Amebainisha kuwa watumishi wa umma hawapaswi kukaa ofisini, kuwataka kupanga siku nne kwa wiki kuwatembelea wananchi hususani waishio maeneo ya vijijini kwa ajili ya kuwasikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi.

Advertisement

Katika ziara hiyo, Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga kumpelekee taarifa za utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya,  Waryoba Gunza baada ya kushindwa kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa mradi wa maji kata ya Rutamba.

Awali,  akizungumza kwa niaba ya wabunge wa mkoa wa Lindi, mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Lulida amesema wakazi wa kata ya Rutamba wanakabiliwa na changamoto ya maji licha ya kuwepo kwa vyanzo, hivyo aliiomba Serikali iwasaidie.

Majaliwa amesema miradi yote ambayo gharama zake ziko chini ya Sh100 milioni inatakiwa itekelezwe kwa kutumia fedha za ndani ya halmashauri husika. “Miundombinu hiyo ilitakiwa iwe imebadilishwa. Mradi wa Sh75 milioni  unaomba fedha wizarani ni uvivu.”

Advertisement