Majina wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza 2020 haya hapa

Muktasari:

Wanafunzi 701,038 sawa na asilimia 92.27 waliofanya mtihani wa darasa la saba mwaka 2019 wamechaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza mwaka 2020.


Dodoma. Wanafunzi 701,038 sawa na asilimia 92.27 waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka 2019 wamechaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza mwaka 2020.

Wakati hao wakipata nafasi, wenzao 58,699 hawakupata nafasi kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa huku ikiagizwa ujenzi wa madarasa ufanyike mapema ili waweze kuendelea na masomo.

Oktoba 15, 2019 Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) lilitangaza matokeo ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019 ambapo asilimia 81.50 ya watahiniwa 933,369  walifaulu huku watahiniwa 909 wakifutiwa matokeo kwa sababu ya udanganyifu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Desemba 5, 2019 Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo amesema waliokosa nafasi wanatoka katika Mikoa 13 nchini huku Mkoa wa Kigoma ukiwa na idadi kubwa ya wanafunzi 12,092. Amesema

waliokosa nafasi ni sawa na asilimia 7.73.

“Wanafunzi 701,038 sawa na asilimia 92.27 watajiunga moja kwa moja kidato cha kwanza Januari 2020 na kati yao  wanafunzi 3,145 sawa na asilimia 0.41 watajiunga na shule za bweni.”

“Kati ya waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wavulana ni 335, 513 na wasichana ni 365, 525,” amesema Jafo.

Waziri Jafo amesema hadi Februari 2020 madarasa yawe yamekamilika ili wanafunzi wajiunge mapema shuleni.