VIDEO: Makamba ataja mambo manne kumpata rais

Makamba ataja mambo manne kumpata rais

Muktasari:

Mbunge mteule wa Bumbuli (CCM), January Makamba amesema ikiwa zimebaki siku nane Watanzania kupiga kura kuchagua rais, wabunge na madiwani kuna mambo manne ya kuzingatia ili kumchagua kiongozi mkuu wa nchi.

 

Korogwe:  Mbunge mteule wa Bumbuli (CCM), January Makamba amesema ikiwa zimebaki siku nane Watanzania kupiga kura kuchagua rais, wabunge na madiwani kuna mambo manne ya kuzingatia ili kumchagua kiongozi mkuu wa nchi.

Ameyataja mambo hayo kuwa ni ubora wa sera, ilani ya uchaguzi, chama na mgombea.

Alieleza hayo leo Jumanne Oktoba 20, 2020 katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa CCM, John Magufuli uliofanyika mjini Korogwe Mkoa wa Tanga.

Amesema wapiga kura lazima waangalie rekodi na historia ya vyama katika kutekeleza ahadi zake nakuongeza kuwa historia ya CCM  ni kuaminiwa katika uongozi wa nchi,  kuongoza  nchi kwa  utulivu na usalama pamoja na ustawi.

Amedai  kati ya vyama vyote vilivyosajiliwa  hakuna hata  kimoja chenye sifa na sura  ya kitaifa  kama CCM huku akiwataka wananchi kuangalia uimara wa mgombea na chama.

"Hata  ukimsikia Rais wetu  Magufuli anavyohutubia kwenye mikutano yake ya kampeni wala hatukani mtu, hamsemi mtu  wala hamlalamikii mtu bali anazungumza  mambo yanayogusa mahitaji  ya wananchi  na hiyo ni sifa nyingine aliyonayo mgombea wetu,” amesema Makamba