Makandarasi wanaidai Serikali ya Tanzania Sh1 trilioni

Muktasari:

  • Ripoti ya  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeeleza kuwa  Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) haukuwalipa makandarasi Sh1.03 trilioni.

Dar es Salaam. Ripoti ya  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeeleza kuwa  Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) haukuwalipa makandarasi Sh1.03 trilioni.

CAG amesema  fedha hizo hazijalipwa  mpaka Novemba,  2019 hali inayoathiri uwezo wa kifedha wa makandarasi na  kuchelewesha ukamilishaji wa miradi hiyo na jamii husika kutonufaika nayo kwa wakati uliokusudiwa.

 “Nimepitia miradi ya ujenzi wa barabara na viwanja vya ndege inayotekelezwa na Tanroads na kubaini madai ya Sh1.03 trilioni kutokana na kucheleweshwa kwa malipo ya hati za madai ya kazi, riba na fidia,” inaeleza ripoti hiyo ya CAG kuhusu miradi ya maendeleo.

Deni hilo limechangiwa na madai ya Sh794.09 bilioni, riba ya kuchelewesha malipo Sh224.02 bilioni na fidia Sh13 bilioni zilizotokana na kutolipwa watu walioathiriwa na miradi iliyotekelezwa.

 

Deni la makandarasi, wahandisi washauri na watu walioathiriwa na miradi, mkaguzi huyo amesema limesababishwa na kuchelewa kwa fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango.

CAG anasema ucheleweshaji wa kulipa madeni hayo unaongeza riba na kusababisha kuongezeka kwa gharama za miradi kinyume na gharama zilizokadiriwa awali.

Kwenye usimamizi wa fedha za miradi iliyotekelezwa na mamlaka nyingine, CAG amesema zaidi ya Sh5.82 bilioni hazikulipwa kwa watu walioathirika na utekelezaji wa Programu ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Usafirishaji Jijini Dar es salaam (DUTP) na Programu ya Kusaidia Sekta ya Usafirishaji (TSSP).

Kutolipwa kwa fedha hizo, amesema kumeathiri mipango ya wananchi waliopisha miradi husika.