Makonda aagiza maduka yote Dar kesho yafunguliwe saa 5 asubuhi

Sunday October 13 2019
makonda pic

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Tanzania, Paul Makonda.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Tanzania, Paul Makonda ameagiza maduka yote kesho yaanze kufunguliwa saa 5 asubuhi  ili kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa vitendo kwa kujiandikisha kwa wingi katika daftari la wapigakura ili kupata fursa ya kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Makonda ametoa agizo hilo leo Jumapili Oktoba 13, 2019 kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari.

 Katika taarifa hiyo, Makonda amesema, "Kesho Oktoba 14 ni kumbukizi ya miaka 20 ya Mwalimu Nyerere tangu atangulie mbele za haki, pia  ni siku ya mwisho ya kujiandikisha katika daftari la wapiga kura. Kwa kukuza demokrasia ndani ya mkoa huu naelekeza maduka yote yafunguliwe kuanzia saa tano asubuhi.

“Baba wa Taifa alithamini viongozi wa mitaa kwa sababu ni nguzo kuu katika uendeshaji wa shughuli za Serikali, tumuenzi kwa kujiandikisha, wafanyabiashara wote wa mkoa huu maduka yenu yatafunguliwa kuanzia saa tano asubuhi kesho,” amesisitiza katika taarifa hiyo.

Hata hivyo, Ofisi ya Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi,) tayari imesema imeongeza siku tatu za uandikishaji na sasa mwisho itakuwa Oktoba 17.

Amewataka wafanyabiashara wanaofungua maduka yao wahakikishe wamejiandikisha huku akiwaomba  wamachinga, waendesha boda boda  na viongozi wa Taasisi za Serikali na binafsi na wanafunzi waliotimiza miaka 18 kutumia fursa ya kesho kujiandikisha.

Advertisement

Mbali na wafanyabiashara wa maduka, Makonda amewataka wamiliki wa baa na sehemu nyingine za starehe kuwahamasisha wanaofika kwenye maeneo yao kujiandikisha kwa kuwa kupiga kura ni haki ya msingi ya kila raia.

 “Ndugu zangu wenye vilabu, baa na sehemu zote za starehe naomba wahamasisheni watu wenu kwenye maeneo yenu kuhakikisha wamejiandikisha.

Kesho miongoni kwa maeneo nitakayoyatembelea ni pamoja na baa, ni matumaini yangu nikifika eneo hili nitakukuta umejiandikisha,” amesema Makonda.

 

Advertisement