VIDEO: Makonda aeleza anakotoa fedha za misaada

Muktasari:

Siku chache baada ya wananchi kuhoji kuhusu chanzo cha fedha ambazo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekuwa akizigawa, ameamua kuweka wazi vyanzo vyake vya fedha anazozitoa kwa jamii mbalimbali kama msaada na zawadi huku akisema uadilifu  na uaminifu wake ndiyo unaofanikisha hayo yote.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda ametaja vyanzo vya fedha ambazo amekuwa akizitoa kwa watu mbalimbali kama msaada na zawadi.

Makonda amesema huwatumia watu wenye kipato kikubwa kuzungumzia matatizo mbalimbali katika jamii na wao hutoa misaada ambayo yeye huiwasilisha kwa wananchi wenye uhitaji.

Akizungumza leo Jumatano Septemba 18, 2019 wakati Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizindua kambi ya upasuaji wa moyo iliyoandaliwa na taasisi ya Shajjah Charity Group kutoka Nchi za Falme za Kiarabu, Makonda amesema watu waache kumzungumzia tofauti na hali halisi ilivyo.

“Mheshimiwa waziri (Ummy) kuna watu wanasema huyu Makonda anatoa wapi  hela, kwa mfano zile fedha milioni 10 za Juma Kaseja zimepigiwa kelele kwelikweli..ooh kapiga penati kapewa milioni 10.”

“Jamani nchi hii ni tajiri na watu wa nchi hii ni tajiri pia, inahitajika tu mtu mwaminifu mwadilifu anayeomba pesa kwa matumizi sahihi na watu wao wanatoa pesa. Balozi huyu wa Falme za Kiarabu yupo ana marafiki wengi lakini huwa namuona wengine wanakunywa naye kahawa basi….” amesema

“Mimi nakaa naye kunywa kahawa lakini huwa namweleza kuna uhitaji wa watoto yatima 500 wapate bima za afya, watoto wa kike 100 wanaosoma masomo ya sayansi kidato cha tano wapate ufadhili wa masomo ,” amesema Makonda.