Masharti ya ununuzi nyumba za PSSSF yapunguzwa makali

Dodoma. Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), uko katika mchakato wa kubadili masharti ya mikataba ya mauzo ya nyumba zake zilizoko Buyuni Chanika jijini Dar es Salaam na miongoni mwa masharti yatakayobadilishwa ni muda wa marejesho.

Nyumba hizo ziliuzwa kwa watumishi wa Serikali chini ya utaratibu wa mteja kupanga na kisha kufanya marejesho hadi deni lake litakapomalizika.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Ajira, Vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama alikaririwa juzi akiamuru kushushwa kwa gharama za nyumba za miradi baada ya kubaini zinauzwa kwa bei kubwa na haziendani na uhalisia wa soko.

Akizungumza na Mwananchi jana, Meneja wa Makazi (Estate Manager) wa mfuko huo, Benedict Mahona alisema kwa sasa muda wa kufanya marejesho hadi kumaliza deni ni miaka 25.

“Hii miaka 25 iliwekwa ili mtumishi awe amemaliza kurejesha kabla ya kustaafu na hivyo anapostaafu aweze kumiliki nyumba lakini sasa tungependa tuziuze kwa muda mfupi zaidi,” alisema Mahona.

Alisema utaratibu utakaoweka masharti yatakayotumika katika mikataba ya mauziano utakamilika mapema na watu watafahamishwa jinsi ya kuzinunua.

“Watumishi ambao tayari walishanunua nyumba hizi chini ya utaratibu huu, hawataondolewa kwenye nyumba bali watapigiwa hesabu kiasi kilichobakia.

Kitachobadilika ni masharti yaliyo katika mkataba ikiwemo muda wa kumalizia marejesho ambao kwa sasa ni miaka 25,” alisema.

Akihitimisha ziara katika mradi huo, Mhagama alisema alifikia uamuzi wa kupunguza bei ya nyumba hizo kutokana na nyumba nyingi kutonunuliwa, gharama za mfuko kuzitunza zinaongezeka huku zikiendelea kuharibika.

Alisema mradi huo wa nyumba za gharama nafuu katika eneo la Buyuni Chanika ambao una nyumba 480 kati ya hizo, 204 hazijapata wanunuzi na 276 malipo yake hayajakamilika.

Mhagama alisema mdodoro wa ununuzi wa nyumba hizo umesababisha makato ya urejeshwaji wa kila mwezi kuwa juu na watumishi wengi kutomudu gharama au bei ya nyumba hizo.

Alisema nyumba 119 zenye vyumba viwili vya kawaida iliyokuwa inauzwa kwa Sh61.1 milioni, imeshushwa hadi Sh36.58 milioni.

Mhagama alisema nyumba 169 zenye vyumba vitatu vya kawaida iliyokuwa ikiuzwa kwa Sh67.26 milioni, itauzwa Sh41.3 milioni.

Alisema nyumba 146 zenye vyumba vitatu, viwili vya kawaida na ‘master bedroom’ zilizokuwa zinauzwa Sh74.34 milioni kila moja sasa zitauzwa Sh46.02 milioni wakati nyumba yenye vyumba vitatu na ‘master bedroom’ iliyokuwa inauzwa Sh83.78 milioni sasa itauzwa Sh61.36 milioni.

Mhagama alitoa mwezi mmoja ili watu wajipange kununua nyumba hizo na kuongeza kuwa soko lake halifungwi kwa watu binafsi nao wanaruhusiwa kuzinunua.

Waziri huyo alionya kuwa nyumba zikikaa muda mrefu zitageuka kuwa magofu hivyo watapoteza fedha za wanachama bila sababu za msingi.

Alisema maagizo hayo yanahusu maeneo mengine yenye miradi hiyo nchini kama Mtwara, Tabora, Morogoro, Iringa hadi Shinyanga.

Mradi huo ulianzishwa mwaka 2011 na kukamilika 2013 ukiwa ni mkakati wa PSPF kabla ya kuwa PSSSF ili kuondoa tatizo la makazi kwa watumishi wa umma.