Mbunge Matiko akiri kumiliki bastola

Wednesday December 4 2019

 

By Pamela Chilongola, MwananchI [email protected]

Dar es Salaam. Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther  Matiko amekiri kumiliki bastola aina ya Revolver yenye risasi tano.

Matiko na viongozi wengine wanane wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 112/2018 yenye mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Matiko ameeleza hayo leo Jumatano Desemba 4, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo,  Thomas Simba wakati akitoa utetezi wake katika kesi hiyo.

Akihojiwa na wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo  Simon kama anamiliki silaha hiyo, mbunge huyo wa Tarime Mjini alikiri kuimiliki.

Alipoulizwa kama silaha hiyo iliwahi kufyatua risasi kati ya  mwaka 2014 hadi 2015,  Matiko amesema hakumbuki.

Matiko ambaye ni shahidi wa tano katika kesi hiyo akiongozwa na wakili wa utetezi, Peter Kibatala amedai  Februari 16, 2018 alipewa kazi na viongozi wake waliokuwa kwenye kamati ndogo ashughulikie masuala ya uchaguzi.

Advertisement

Amesema masuala hayo ni  barua za utambulisho pamoja na nakala za viapo za mawakala wa kusimamia uchaguzi jimbo la Kinondoni.

"Mawakala wetu hadi inafika Februari 16, 2018 walikuwa hawajapewa barua za utambulisho pamoja na nakala za viapo. Walitakiwa wapewe siku saba nyuma ndipo tukaelezwa na viongozi wetu tulifuatilie suala hilo lakini halikuleta matunda hadi Februari 17, 2018 ulipofanyika uchaguzi,” amedai Matiko.

Mbali na Matiko na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Bara); Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini); Halima Mdee (Kawe); John Heche(Tarime Vijijini); Ester Bulaya (Bunda) na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

Advertisement