Mbunge Mtulia aanza amshaamsha kuelekea uchaguzi serikali za mitaa

Muktasari:

  • Mbunge wa Kinondoni (CCM), Maulid Mtulia amewataka wanaCCM na wananchi kujiandikisha kwa wingi kuelekea uchaguzi ya serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Dar es Salaam. Mbunge wa Kinondoni (CCM), Dar es Salaam nchini Tanzania, Maulid Mtulia amewataka wananchi kujiandikisha na kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Mtulia amewasisitiza wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea kwenye uchaguzi huo.

Mbunge huyo ameyasema hayo leo Jumapili Septemba 22, 2019 katika kongamano la Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Ndugumbi wilaya ya Kinondoni lililoambatana na uzinduzi wa mashina.

Amesema hamasa kubwa inatolewa kwa wanachama wanawake wagombee kwenye uchaguzi huo wa serikali za mitaa, kwa kuwa chaguzi nyingi wanawake wanakuwa nyuma kwenye kugombea

"Kama unavyojua wanawake wako active lakini kwenye kugombea wanakuwa nyuma hivyo tumeamua kuja kuwahamasisha huku kwenye mashina.”

“Wapo viongozi wengi wanawake waliopita waliofanya vizuri sana kwenye uongozi kama kina Bibi Titi, hivyo tunawaomba wanawake wasiogope" amesema Mtulia

 

Mtulia amesema lengo ni kuimarisha wanachama ili kuhakikisha uchaguzi wa serikali za mitaa CCM inapata ushindi mitaa yote.

Kuhusu changamoto za miundombinu, Mtulia amesema anashirikiana na  Serikali kutatua utatuzi wa changamoto hasa maeneo korofi katika jimbo hilo.

Amesema ili lengo la demokrasia nchini litimie ni pamoja na kuwaelimisha wananchi juu ya haki ya kushiriki kwa wingi katika uchaguzi.

"Kama mnavyojua nchi yetu ni ya demokrasia na ili demokrasia itimie ni pamoja na kuwaelimisha wananchi namna ya kushiriki katika uchaguzi na ili hata kama mtu akishinda anaonekana kweli ameshinda kwa kuchaguliwa na wananchi wengi," amesema

"Haina maana kuwa mtu anashinda kwa kuchaguliwa na watu kumi ni vizuri mtu akishinda anaonekana ameshinda kwa kura nyingi,” amesema

Kwa upende wake, Diwani wa Ndugumi (CCM), Thadei Masawe amesema hamasa hiyo ni mkakati wa kuhakikisha wananchi wanajiandikisha kwa wingi kuelekea uchaguzi huo.

"Sisi tuna kauli mbiu yetu inasema ‘Kituo kinachofuata ni kujiandikisha’ hii itawasaidia wanachama na wananchi kujiandikisha na sio kujiandikisha tu ni pamoja na kupiga kura," amesema Masawe