Mbunge wa CUF amchongea waziri wa Zanzibar kwa PM

Muktasari:


Mbunge wa Konde nchini Tanzania (CUF) Khatib Said Haji amemuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kumchukulia hatua Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Zanzibar, Salama Aboud Tulib kwa kukataa kukaa karantini mara baada ya kuwasili nchini akitokea nje ya nchi.

Dodoma. Mbunge wa Konde Nchini Tanzania (CUF) Khatib Said Haji ameiomba Serikali kumchukulia hatua Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Salama Aboud Talib aliyekataa kukaa kwenye karantini na kusababisha maambukizi kwa watu wawili kwenye familia yake.


Akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2020/2021 amesema matokeo ya Hilo nyumbani kwake kuna watu wawili amewaambukiza na huko hospitali haijulikani matokeo yake nini.
“Ndani ya siku tatu ameng’ang’ana kukaa hospitali ya Mnazi Mmoja matokeo yake akatolewa kwa nguvu baada ya kuona jambo hili limekuwa kubwa sana. Baada ya malalamiko makubwa ndio alikubali kuwekwa kwenye karantini,”amesema.
Amesema alifanya hivyo kwa sababu ya kiburi cha madaraka yake na kumpongeza makamu wa pilli wa Rais Zanzibar kwa kukubali kukaa karantini alipotoka nje ya nchi bila kulazimishwa.
“Huu ndio utu, huu ndio ubinadamu leo waziri huyu ni nani anayekataa uamuzi wa Serikali hata uamuzi wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hatuwezi kumchekea mtu mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu ni waziri ulichukulie hatua haraka. Leo hii baada ya kiburi kingine kuna mtu mwingine ni daktari anaitwa Hafidh hadi leo ameng'ang'ana pale Hospitali ya Mnazi mmoja kwa sababu ana unasaba wa kiukubwa.”
“Uheshimiwa wake ni kwa sababu ana uhai anapumua dakika moja akifumba macho anakuwa marehemu. Taharuki iliyopo pale Mnazi mmoja baada ya matukio hayo ni kubwa. Nataka mheshimiwa ufuatilie kama huyu daktari bado yupo,”amesema.
Amesema kauli anazozitoa katika mtandao ya jamii ni utasema hakuna yoyote anayeweza kumfanya lolote
haya madhara yakianza mahali pamoja yanaenea.