Mchungaji Msigwa achaguliwa uenyekiti Chadema Kanda ya Nyasa

Muktasari:

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amechaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Nyasa akibainisha kuwa safari ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini kuiondoa CCM madarakani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 imeiva.

Mbeya. Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amechaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Nyasa akibainisha kuwa safari ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini kuiondoa CCM madarakani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 imeiva.

Msigwa ametoa kauli hiyo leo Desemba Mosi, 2019 wakati akiwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu wa Chadema Kanda ya Nyasa kwa kumchagua.

Msigwa ameibuka mshindi baada ya kupata kura 66 sawa na asilimia 62.5 kati ya kura 107 zilizopigwa na kuwashinda wapinzani wake,  wakili Boniface Mwabukusi  aliyepata kura 26 na Sadrick Malila ‘Ikuwo’(14).

Amesema baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo wanaelekeza nguvu kuimarisha misingi imara ya chama hicho ikiwa pamoja na kujenga umoja na mshikamo kuhakikisha viongozi wa kanda hiyo hawayumbishwi kwa kurubuniwa.

 “Niwashukuru sana wajumbe wenzangu kwa kuniamini na kunipa ridhaa hii. Najua mzigo nilioongezewa  lakini niwahakikishie hiki chama kitajengwa na wenye moyo wa kujitoa na kusema hadharani bila woga.”

“Adui yetu ni CCM tunapaswa kupambana naye kuanzia sasa na uchaguzi ujao ni mwepesi kwa kuwa kanda yetu hii safu (ya uongozi) mliyotupa ina watu makini,” amsema Msigwa.