Messi alilia Neymar arudi Barcelona

Muktasari:

Lionel Messi ameweka wazi kuwa hakuumizwa na kushindikana kwa dili ya Neymar kurejea Barcelona licha ya kumkubali nyota huyo wa kimataifa wa Brazil.

Madrid, Hispania. Nahodha wa FC Barcelona, Lionel Messi amesisitiza kuwa hakuumizwa na kitendo cha klabu yake kushindwa kumrejesha nyumbani, Neymar msimu huu.

Neymar alicheza kwa mafanikio zaidi na Messi na Luis Suarez na kuunda utatu, uitwao MSN ndani ya Camp Nou ulitikisa soka la Ulaya.

Utatu huo, ulimudu pamoja kuiongioza FC Barcelona kwenye idara yao ya ushambuliaji na kutwaa makombe mawili ya Ligi Kuu Hispania 'La Liga' ndani ya miaka yao mitatu huku pia wakibeba Copa del Rey na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2014-15.

Muunganiko wao, ulivunjika 2017 wakati Neymar aliamua kuondoka Camp Nou kwa kujiunga na Paris Saint-Germain kwa rekodi ya Euro 222milioni.

Hata hivyo, majira haya ya kiangazi iliripotiwa kuwa nyota huyo wa Kibrazili alikuwa tayari kuondoka Parc des Princes kwa kurejea Hispania lakini ilishindikana kutokana na kushindwa kufikiana makubaliano kati ya FC Barcelona na PSG.

"Nilipenda kuona Neymar anarejea. Binafsi, sijui kama Barca walifanya kila linalowezekana kumfanya akarejea, lakini nafahamu kama kuwasahawishi PSG wamwachie sio jambo jepesi," alisema Messi.

Messi aliendelea; "Sijaumizwa na kilichotokea. Tunatimu nzuri yenye uwezo wa kukabiliana na yeyote, bila ya yeye lakini ukimzungumzi ni kati ya wachezaji bora kwa sasa Duniani."

Kufuatia uwepo wa tetesi kwamba Messi alikuwa akishinikiza kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kuwa wanataka kuona FC Barcelona wakimrejesha Neymar taarifa hizo amezikanusha.

"Hatujawahi kushinikiza kuwa Neymar asajiliwe, yalikuwa ni mawazo yetu tu," alisema Messi.