Mkapa aeleza alivyowagomea waliotaka abadili ukomo wa urais

Rais Mstaafu Benjamin Mkapa akimkabidhi nakala ya kitabu chake mfanyabiashara, Atlaf Hirani baada ya kukitambulisha katika mikoa ya Kanda ya Ziwa katika sherehe iliyofanyika jijini Mwanza juzi. Na Mpigapicha Wetu

Mwanza. Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa amefichua jinsi baadhi ya wazee wa Zanzibar walivyomtembelea kumshawishi aruhusu mabadiliko ya katiba kumwezesha aliyekuwa Rais wa Zanzibar wakati huo kuongoza kwa awamu tatu badala ya mbili za kikatiba.

Akizungumza jijini Mwanza juzi wakati wa hafla ya kutambulisha kitabu chake, Mkapa alisema suala hilo lilikuwa kiunzi ambacho kilikaribia kumuingiza kwenye mtikisiko kiuongozi.

“Nilikaribia kupata mtikisiko lakini nilifanikiwa kuruka kiunzi hicho ingawa ilikuwa kazi nzito kweli. Tulizungumza kwa makini na hatimaye tulielewana; na katiba ya Zanzibar ikabaki na vipindi viwili vya miaka mitano kama ilivyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano,” alisema

Alisema kufanikiwa kuruka kiunzi hicho ni miongoni mwa mambo anayojivunia na kuona ufahari kwa sababu aliweza kulinda Katiba ya Zanzibar na ile ya Muungano hadi alipokabidhi kijiti cha uongozi kwa Rais Jakaya Kikwete.

Alisema anafurahi kuona msingi wa uongozi unaolinda na kuheshimu katika kupokezana vijiti unaendelea kuheshimiwa na viongozi waliofuata baada ya Kikwete naye kumkabidhi kijiti Rais John Magufuli.

“Mungu ampe (Magufuli) afya njema aongoze awamu mbili (ya miaka mitano mitano kwa mujibu wa katiba); nina hakika hatataka kuongeza awamu ya tatu,” alisema Mkapa.

JPM askari wa mwamvuli

Alitumia nafasi hiyo kuelezea jinsi alivyomteua na kumwingiza Rais Magufuli katika baraza lake la mawaziri huku akimmwagia sifa kwa uchapa kazi aliouonyesha na ameendelea kuonyesha hata sasa akiwa rais.

“Nilipounda Baraza la Mawaziri nililolipachika jina la “Askari wa mwamvuli” John Magufuli alikuwa miongoni mwao akiwa (naibu) waziri wa ujenzi alikoleta mabadiliko makubwa. Watu wa Kusini hawatamsahau kwa ujenzi wa Daraja la Mkapa pale Mto Rufiji ambalo kwa kweli lilistahili kuitwa Daraja la Magufuli,” alisema Mkapa.

Alisema akiwa katika nafasi yake ya uwaziri wa ujenzi wakati huo, Rais Magufuli alimshauri kuacha kutegemea wahisani kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, badala yake Serikali ianze kutumia fedha na rasilimali za ndani kutekeleza miradi hiyo.

“Nikamkubalia ushauri huo na tulipokwenda kwenye Baraza la Mawaziri, niliagiza tuanze kutenga kiasi fulani cha fedha kila mwezi kwa ajili ya ujenzi wa barabara,” alisema.

Alisema ana imani na uwezo wa kiuongozi, uthubutu na utendaji kazi wa Rais Magufuli na amewashukuru Watanzania kwa kumchagua kuongoza awamu ya tano.

Nyerere na ubinafsishaji

Akihutubia hafla hiyo iliyoandaliwa na Benki ya NMB, alikumbushia alivyoendesha ubinafsishaji wa mashirika, makampuni na viwanda vya umma kinyume na mapenzi ya Mwalimu Julius Nyerere.

Alisema Baba wa Taifa hakupenda ubinafsishaji lakini hapakuwa na namna, maana mashirika mengi yalishindwa kujiendesha wakatafuta namna ya kuyaokoa.

“Nilitaka kudhihirisha kwamba maendeleo yanaweza kuletwa na wote; sekta binafsi pamoja na Serikali,” aliongeza.

Akigusia yaliyomo kwenye kitabu chake cha “My Life My Purpose” Mkapa alisema, “kuna mambo ambayo sekta binafsi haiwezi kuyafanya....hayo yatafanywa na Serikali. Lakini kwenye elimu huwezi kumzuia mtu binafsi kuanzisha chuo. Haya mambo yanategemeana.”

Alitaja moja mafanikio ya ubinafsishaji kuwa ni kuundwa kwa Benki ya NMB mwaka 1997 baada ya kugawanywa kwa iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).

“Nafarijika kuona NMB ni miongoni mwa mabenki makubwa yenye mtandao mkubwa nchini ikihudumia wananchi wa kawaida hadi vijijini,” alisema Mkapa.

Akizungumzia mafanikio ya benki hiyo, Kaimu Mkurgenzi Mtendaji wa NMB, Ruth Zaipuna alisema kwa kipindi cha miaka 22 iliyopita, benki hiyo imejipambanua kuwa kimbilio la wafanyabiashara wadogo, kati na wakubwa kwa mitaji na ushauri wa kitaalam.

Alizuia helikopta kwenye kampeni

Huku akizungumza kwa ucheshi na bashaha, kiongozi huyo mstaafu pia alifichua siri jinsi Mwalimu Nyerere alivyozuia mpango wa timu ya kampeni ya CCM ya kutumia usafiri wa helikopta kumnadi wakati wa kampeni za mwaka 1995.

“Alikuwa China wakati alipoambiwa kwamba timu ya kampeni inafikiria tukodishe helkopita ya kufanyia kampeni. Alipiga simu Ofisi ya Rais kukataa kwa hoja kwamba wapiga kura wanatakiwa wanione na kunisikiliza na siyo kurukaruka kwa helikopta,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kusisitiza kuwa Nyerere hakumwandaa kuwa Rais kama wengi wanavyodhani, bali baada ya kuteuliwa aliunga mkono uteuzi na kuzunguka sehemu mbalimbali kumnadi.