Moto tena bweni la shule ya Kiislamu

Muktasari:

Bweni hilo la shule ya mafundisho ya dini katika wilaya ya Hai iliungua Ijumaa ya Oktoba 16 na wanafunzi watatu wa shule hiyo wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano.

Moshi. Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, amewaagiza polisi kuwahoji kwa kina wanafunzi watatu wanaowashikilia kwa kuchoma bweni la shule ya dini ya Kiislamu ya Othuman Bin Hassan.

Sabaya ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, alisema jengo hilo lilichomwa Ijumaa ya wiki iliyopita, lakini maelezo ya wanafunzi hayo bado yana utata.

 

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Oktoba 18,2020, mkuu huyo wa wilaya alidai baada ya wanafunzi hao kuhojiwa, alidai kiini cha wao kuchoma jengo hilo ni kujaribu kushawishi kufungwa kwa shule.

“Tumekamata watu watatu waliochoma bweni la shule ya Kiislamu . Hao vijana watatu waliiba simu huko ndani. Waliiba simu 68 walipoiba hizo simu wakazificha juu ya dari hapo shuleni,” amesema Sabaya.

 “Kwa maelezo yao waliona wachome ili shule ifungwe ili watoweke na hizo simu. Nimewaambia polisi waendelee kuwahoji vizuri kwa sababu hayo maelezo yanaonekana kama hayaungani,” alisisitiza Sabaya.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Emanuel Lukula alipotafutwa kwa simu kuulizwa juu ya matukio hayo amesema hawezi kuyazungumzia kwa sababu yuko kwenye msafara hadi atakaporejea ofisini.

Hii inakuwa shule ya 3 ya taasisi ya dini ya Kiislamu kukumbwa na matukio ya moto huku ya karibuni kabisa ikiwa ni shule ya sekondari ya Uchira Islamic iliyopo Uchira iliyoungua usiku wa Ijumaa iliyopita.

Shule nyingine ambazo zimeshaungua ni Kaloleni Islamic iliyopo Kaloleni ambayo imeungua mara mbili na tukio la karibuni kabisa lilitokea usiku wa Oktoba 8 na kusababisha bweni lenye jengo la ghorofa kuungua.