DC Odunga ashindwa kufika mahakamani kusikiliza rufaa kupinga kutoa Sh7 milioni za matunzo ya mwanaye

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga leo Jumanne Novemba 19, 2019 ameshindwa kufika katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kusikiliza rufaa aliyokata kupinga hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Ukonga.

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga leo Jumanne Novemba 19, 2019 ameshindwa kufika katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kusikiliza rufaa aliyokata kupinga hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Ukonga.

Katika hukumu hiyo, Odunga alitakiwa kutoa Sh7 milioni kama nusu ya gharama za matunzo aliyotumia mkewe, Medelina Mbuwuli kumsomesha mtoto wao kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita.

Odunga alifungua kesi kumtaliki mkewe lakini mahakama ililikataa ombi hilo, badala yake ikamtaka alipe kiasi hicho cha fedha.

Rufaa hiyo leo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Glory Nkwera na kutokana na mkuu huyo wa wilaya kutokuwepo mahakamani, hakimu huyo aliahirisha kuisikiliza hadi Desemba 12, 2019.

Katika maelezo ya kukata rufaa, Odunga alidai kuwa hakimu aliyesikiliza kesi yake dhidi ya Medilina alifanya kosa kutamka amlipe Sh7 milioni.

Alisema hakimu huyo alifanya kosa kwa kutokutoa talaka na kubainisha kuwa ana imani ndoa yake haipo.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa Oktoba 18, 2019  na Hakimu Christina Luguru baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na pande zote mbili alisema mdaiwa aliiomba mahakama kuwa Odunga atoe nusu ya Sh13 milioni ambazo alitumia kumhudumia mtoto wao na aendelee kuwatunza yeye na mwanaye kwa kuwa bado ni mkewe.

Hakimu Luguru alisema sheria ya ndoa kifungu cha 63 inaeleza pamoja na kifungu cha 129 ni jukumu la baba kutunza mke na mtoto. Alisema kwa ushahidi uliotolewa kwenye kesi hiyo, umeonyesha mtoto wao bado anasoma na mdai hakuwa akitoa matunzo hadi kupelekwa polisi.

Odunga hakuwa na ushahidi wowote kuonyesha alikuwa akilipa ada ila mdaiwa alipeleka risiti za ada mahakamani zikionyesha alilipa Sh14 milioni.

Katika kesi hiyo, mwanamke huyo alikuwa anadai kuwa mumewe hajawahi kutoa matunzo ya mtoto wao wa kike mwenye miaka 18 tangu akiwa chekechea hadi sasa yupo kidato cha sita.

Alisema licha ya mumewe kutotoa matunzo hayo, hayupo tayari kupewa talaka kwa sababu ndoa yao ni takatifu ya kanisani na bado anampenda mume wake na kwamba anajua hizo ni changamoto tu zimempitia.