Polisi yataja sababu kuzuia mkutano wa Mchungaji Msigwa

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoani Iringa limetaja sababu nne za kuzuia mkutano wa hadhara wa mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.

Dar/Iringa. Jeshi la Polisi mkoani Iringa limetaja sababu nne za kuzuia mkutano wa hadhara wa mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.

Moja  ya sababu ni kupata taarifa za kiintelijensia zinazohusisha kundi la watu waliopanga kufanya vurugu katika mkutano huo.

Barua  ya Jeshi la Polisi Wilaya ya Iringa inaeleza kuwa Oktoba 22, 2019 Mchungaji Msigwa alitoa taarifa za kufanya mkutano na wananchi uwanja wa Mwembetogwa kesho Jumamosi Oktoba 26, 2019 na kuzuia mkutano huo.

Akizungumza na Mwananchi, mbunge huyo amesema zuio hilo halijamuathiri kisiasa na badala yake linamtengenezea ushawishi mkubwa wa kufanya mkutano ujao.

Amesema hoja zilizotolewa na Polisi hazina mashiko katika hitaji lake la kuzungumza na wananchi.

“Ni mikutano mingi sana nimezuiliwa ambayo sina kumbukumbu ya idadi yake. Wananizuia kwa sababu ukweli wanaufahamu na hawataki wananchi wapate taarifa hizo lakini wananchi kwa sasa wanahitaji kuelezwa ukweli ili kufanya uamuzi,”amesema Msigwa.

Katika barua ya zuio hilo, Kamanda wa Wilaya ya Iringa, Hamad Mauod ametaja sababu nyingine ni kutokuwapo kwa askari wa kutosha kusimamia mkutano huo kwa maelezo kuwa nguvu imeelekezwa katika usimamizi wa usimamizi wa mitihani ya kidato cha nne, pili na darasa la nne.

Kamanda huyo amesema sababu nyingine ni dalili za kuanza kampeni mapema za kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa kabla ya kalenda ya kampeni kuanza.

Kamanda huyo amebainisha kuwa sababu nyingine ni barua ya mkutano huo kutoweka wazi dhumuni la mkutano ikiwa ni kinyume cha kifungu cha 43(1)(b) cha Sheria ya Polisi na Polisi wasaidizi sura 322 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

“Kwa hiyo Jeshi la Polisi halipaswi kufanya kazi kwa kufuata matakwa ya viongozi bali linafanya kazi kwa weledi ikiwa ni pamoja na kutenda haki kwa wananchi, kufuata misingi ya majukumu bila kutumika kisiasa,” amesema Kamanda Masoud.